November 24, 2024

CPJ wadai wafanyakazi wao wawili wanashikiliwa Tanzania

Yaeleza kuwa walikamatwa wakiwa hotelini jijini Dar es Salaam Jumatano hii na kupelekwa kusikojulikana.

Wafanyakazi wa Kamati ya Kutetea Wanahabari Duniani (CPJ) Muthoki Mumo (kushoto) na Angela Quintal wanaodaiwa kushikiliwa na maofisa wanaodaiwa kutoka Idara ya Uhamiaji. Picha|CPJ.


  • Idara ya uhamiaji imesema inafuatilia kwa kina taarifa hizo kujua ukweli wake.
  • CPJ inadai moafisa waliojitambulisha kuwa wanatokea uhamiaji waliwapekua na kuwanyang’anya pasi za kusafiria.

Dar es Salaam. Kamati ya Kutetea Wanahabari Duniani (CPJ) imesema kuwa wafanyakazi wake wawili wamekamatwa na watu wanaodaiwa kuwa ni maofisa wa Idara ya Uhamiaji nchini wakiwa katika shughuli zao za kikazi jijini hapa, taarifa ambayo Serikali imesema “inaifuatilia kwa kina”.

Taarifa ya CPJ iliyochapishwa katika tovuti yao inaeleza kuwa Mratibu wa Programu wa Afrika Angela Quintal na Mwakilishi wa kamati hiyo ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, Muthoki Mumo walikamatwa jana jioni wakiwa hotelini walikofikia.

Taarifa hiyo inasema maofisa hao walipekua mali zao na hawakutaka kurudisha pasi zao kusafiria na baadaye waliwachukua Quintal na Mumo kutoka hotelini na kupelekwa mahali ambapo hapajulikani.

“Tunaguswa na usalama wa wenzetu Angela Quintal na Muthoki Mumo ambao walizuiliwa na mamlaka wakiwa Tanzania kihalali,” amesema Joel Simon, Mkurugenzi Mtendaji wa CPJ.

“Tunazisihi mamlaka husika kuwaachia haraka na kurejesha pasi zao za kusafiria.”

CPJ imeeleza kuwa Quintal na Mumo walikuwa katika majukumu yao ya kikazi nchini lakini haijaweka bayana walikuwepo kwa kipindi gani.


Zinazohusiana: MCT wajitosa kuongeza idadi ya wanawake kuripoti habari za kilimo


Hata hivyo, Idara ya uhamiaji imeeleza kuwa haina taarifa rasmi za kukamatwa watumishi hao na kwamba inafuatilia kwa kina.

Msemaji Mkuu wa idara hiyo, Ali Mtanda ameiambia Nukta kuwa wanaendelea kufuatilia tukio hilo kama lipo kwa kuwa nao wameona kwenye vyombo vya habari na mitandao.

“Tunafuatilia kwa kina kujua ni chombo gani cha dola kimewakamata kama ni polisi ama uhamiaji kama inavyodaiwa.

“Hata kama walikamatwa na uhamiaji na jambo hili lililotokea jana kuna utaratibu wa hizi ripoti kuifikia ofisi ya Kamishna Jenerali ndiyo maana hatufahamu hivyo hadi mchana tunaweza kuwa na taarifa kamili,” amesema Mtanda.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa ofisi yake inafuatilia kujua kwanini wanaoitwa Waandishi wa habari wa CPJ waliruhusiwa na baadaye wakalazimika kuhojiwa na uhamiaji.