October 6, 2024

Dar yaongoza kupata sifuri matokeo kidato sita

Kati ya wanafunzi 674 waliopata daraja sifuri, asilimia 13.9 wanatoka mkoa huo.

Muonekano wa jiji la Dar es Salaam. Picha|Mtandao


  • Kati ya wanafunzi 674 waliopata daraja sifuri, asilimia 13.9 wanatoka mkoa huo. 
  • Pia imetoa wanafunzi wengi waliopata daraja la nne.
  • Lindi yavunja rekodi kwa kutokuwa na mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja sifuri.
  • Matokeo hayo yawapa tafakari viongozi na wazazi wa mkoa huo.

Dar es Salaam. Wakati joto la matokeo ya kidato cha sita likiwa bado halijashuka, viongozi na wazazi wa mkoa wa Dar es Salaam watakuwa na kibarua kigumu cha kuinua elimu ya mkoa huo kutokana na matokeo mabovu yaliyopatikana katika mtihani wa mwaka huu. 

Katika matokeo yaliyotangazwa juzi (Julai 11, 2019) na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) Dk Charles Msonde yanaonyesha ufaulu wa jumla umeongezeka kwa asilimia 0.74 ukilinganisha na mwaka jana. 

Katika matokeo hayo Dar es Salaam iko miongoni mwa mikoa iliyofanya vibaya kitaifa, jambo linaloacha tafakari ya kina kwa viongozi kuangalia namna ya kuinua ubora wa elimu ya wanafunzi wake. 

Licha ya Dar es Salaam kuwa miongoni mwa mikoa 10 iliyofanya vibaya kitaifa, ndiyo mkoa wenye idadi ya juu ya wanafunzi waliopata daraja sifuri yaani la mwisho (walioferi kabisa). 

Kwa mujibu wa mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu katika matokeo hayo, watahiniwa 94 wa Dar es Salaam wamepata daraja sifuri sawa na asilimia 13.9 ya waliopata daraja hilo katika mikoa yote ambao walikuwa 674. 

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila wanafunzi 100 waliopata daraja sifuri basi 14 wanatoka mkoa wa Dar es Salaam ambao ulikuwa na shule 61 zilizoshiriki mtihani huo uliofanyika Mei mwaka huu. 

Mkoa wa Mara umekuwa wa pili kwa kuwa na sifuri nyingi zinazofikia 61 ukifuatiwa na Kilimanjaro (56) na Mwanza (54). 

Dar es Salaam imeangushwa na mkoa wa Lindi ambao hauna  mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja sifuri licha ya kukabiliwa na changamoto za miundombinu ya utoaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu.


Soma zaidi: 


 Pia imeongoza kuwa na wanafunzi wengi waliopata daraja la nne ambalo ni la pili kutoka mwisho la walioferi kabisa. 

Waliopata daraja la nne katika mkoa huo ni 246 na kufuatiwa kwa mbali na Mwanza (169); mkoa ambao uko miongoni mwa mikoa 10 ya mwisho kitaifa. 

Licha ya matokeo mabovu ya Dar es Salaam, imefanikiwa kuingiza shule tatu katika orodha ya shule 10 bora kitaifa. Shule hizo ni Feza Boys, Feza Girls na Canossa zikiungana na shule nyingine za Kisimiri (Arusha), Ahmes (Pwani) na Mwandet (Arusha).

Shule nyingine ni Tabora Boys(Tabora) na Kibaha (Pwani). ,St Mary’s Mazinde Juu (Tanga) na  Kemebos ( Kagera).Pia haijaingiza shule hata moja katika orodha ya shule zilizoshika mkia kitaifa. 

Lakini bado matokeo ya mkoa huo yanafikirisha hasa kwa viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia elimu kuhakikisha wanautoa mkoa huo katika matokeo mabovu ya mwaka huu.