Dk Mpango awaonya wanaotumia fedha za umma vibaya
Amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria.
- Amesema Serikali itawachukulia hatua kali za kisheria.
- Ayataka mabaraza ya madiwani kusimamia vizuri fedha miradi ya maendeleo.
Dar es Salaam. Siku chache baada ya Dk Philip Mpango kuchaguliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, ameonya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa watumishi wa umma watakaojihusisha na vitendo vya ufisadi, ubadhirifu wa fedha za umma utakaoisababishia Serikali hasara.
Dk Mpango ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Buhigwe mkoani Kigoma, ni miongoni mwa waziri wa mwanzo kuchaguliwa na Rais John Magufuli kuingia katika Baraza la Mawaziri katika Serikali ya awamu ya sita.
Mpaka sasa baraza hilo lina mawaziri wawili akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof Palamagamba Kabudi.
Waziri Mpango aliyekua akizungumza Novemba 25, 2020 na wananchi wa kata ya Mnanila mkoani Kigoma amesema watumishi wa umma wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili kuwatumikia vema wananchi.
“Hao mafisadi na wabadhirifu wa fedha za umma nawaonea huruma kwa sababu kisu nimepewa mwenyewe na Waziri wa Fedha hana mipaka, popote ilipo fedha na mali ya umma, akawapo mwizi, mbadhirifu, huyo ni halali yangu” amesema Dk Mpango.
Soma zaidi:
Aidha, ameyaagiza mabaraza ya madiwani kote nchini, kuhakikisha kuwa fedha za miradi zinazotumwa na Serikali katika maeneo yao zinasimamiwa vizuri ili kuleta tija na maendeleo ya jamii.
“Kwa hiyo lazima tufanye kazi ya kukusanya mapato na kutumia fedha vizuri ili watumishi hawa wanaohangaika kila siku na walau wapate kamshahara ambako kanasaidia zaidi” amesisitiza waziri huyo.