November 24, 2024

Dodoma mbioni kupata hospitali inayotembea

Ni basi ambalo lina vifaa tiba na madaktari wabobezi litakalokuwa linatoa huduma za afya katika maeneo yasiyo na vituo vya afya katika mkoa huo.

  • Ni basi ambalo lina vifaa tiba na madaktari wabobezi litakalokuwa linatoa huduma za afya katika mkoa huo.
  • Litakuwa linasimamiwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa na kipaumbele kitakuwa ni maeneo yasiyo na vituo vya afya.
  • Litatolewa na Chama cha Uchumi wa Afrika na Maendeleo Japan (AFRECO). 

Dar es Salaam. Chama cha Uchumi wa Afrika na Maendeleo Japan (AFRECO) imeahidi kuipatia Hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) basi ambalo ni hospitali kamili litakalotoa huduma za matibabu kwa mkoa wa Dodoma.

Basi hilo litakapowasili nchini kutoka Japan linatarajiwa kuwa ni mkombozi kwa wananchi waishio vijijini na katika maeneo ambayo hayana hospitali kwani kila litakakokwenda kutoa huduma litakuwa na madaktari waliobobea katika utaalamu wa tiba mbalimbali, vifaa tiba, maabara pamoja na dawa.

Rais wa AFRECO, Tetsuro Yano ametoa ahadi hiyo leo (Septemba 1, 2019) katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yaliyofanyika kwenye hoteli ya Yokohama Bay nchini Japan.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Yano amesema wameamua kuanza kutoa misaada na huduma zao nchini Tanzania baada ya kufurahishwa na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Ameongeza kuwa anaamini siku moja Tanzania itakuwa nchi ya mfano kwa Afrika Mashariki na Afrika yote kwa kutoa huduma bora za tiba kwani itakuwa na vituo vingi vya afya na hospitali zenye uwezo wa kutibu magonjwa kama vile ya moyo na figo. 

AFRECO ni taasisi inayoziunganisha nchi za Afrika na Japan katika kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na utamaduni.


Zinahusiana:


Waziri Mkuu, Majaliwa amesema mbali na kutoa basi ambalo litakuwa linatoa huduma za matibabu, pia taasisi hiyo ya AFRECO   itasaidia katika kupandisha hadhi hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa shule kamili ya tiba.

Amesema hospitali hiyo ya Benjamin Mkapa  itapatiwa vifaa   mbalimbali vya tiba ambavyo vitaifanya hospitali hiyo kuwa ni shule bobezi   kwa utoaji wa tiba mbalimbali nchini Tanzania na barani Afrika.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa wamekubaliana na AFRECO kuanzisha kitivo maalum cha Uhandisi wa Vifaa Tiba ambacho kitafundisha uhandisi wa vifaa tiba ili nchi yetu iwe na watalaamu wa  kukarabati vifaa tiba pindi vinapoharibika badala kuvipeleka nje ya nchi au kuagiza wahandisi na watalaamu kutoka nje ya nchi kuja kuvitengeneza.

“Hivi sasa yanafanyika makubaliano ya kuanzisha   kiwanda cha kutengeneza vifaa tiba na kwa kuanzia wataanza kutengeneza maji ya drip ambayo huongezwa kwa wagonjwa kwa maeelekezo ya madaktari na baadae watengeneza dawa mbalimbali,” amesema Majaliwa katika taarifa hiyo.