Dodoma yazidi kupaa usafiri wa anga Tanzania
Shughuli za ndege zimeongezeka katika kiwanja cha ndege cha Dodoma mwaka 2017 kwa asilimia 49.2.
- Shughuli za ndege zimeongezeka katika kiwanja cha ndege cha Dodoma mwaka 2017 kwa asilimia 49.2 ukilinganisha na mwaka 2016.
- Kiwanja cha ndege Dodoma ni kiwanja cha saba kwa kuwa na abiria wengi nchini.
Dar es Salaam. Uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma na kuanzisha safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) umeanza kuleta matunda katika mkoa huo kwa kufungua fursa lukuki ambazo hapo awali zingeweza kuchukua muda kufikiwa.
Jambo la kujivunia kwa wakazi hao ni maboresho makubwa yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wa jiji hilo ambalo ndiyo mji mkuu wa Tanzania ambapo ndege zinaweza kutua na kupaa saa 24.
Hali hiyo imefanya uwanja wa Dodoma kuwa miongoni mwa viwanja 10 nchini ambavyo ndege nyingi zinatua na kuruka, hiyo ni kwa mujibu wa Ripoti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) ya mwaka 2017.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa shughuli hizo za ndege zimeongezeka mpaka kufikia ndege 4,004 mwaka 2017 sawa na asilimia 49.2 ukilinganisha na ndege 2,682 zilizoruka na kutua mwaka 2016.
Takwimu hizo za TAA zinaeleza zaidi kuwa Aprili na Mei 2017 ndiyo miezi ambayo ilikuwa na shughuli nyingi zaidi (busy) katika mwaka huo. Aprili mwaka huo ndege zilifanya safari zake mara 423 na kupaa kidogo mwezi uliofuata wa Mei ambapo ndege ziliruka na kutua mara 435.
Hali hiyo pia imekifanya kiwanja cha ndege cha Dodoma kushika nafasi ya saba kati ya viwanja 10 nchini vinavyopokea wageni wengi huku kikishika nafasi ya sita kwa viwanja vya ndege vinavyoongoza kwa ndege nyingi za kutua na kuruka hapa nchini.
Kiwanja hicho kimefanikiwa pia kurekodi abiria 31,605 ambao walitumia kiwanja hicho kwa mwaka 2017 ikiwa ni karibu mara mbili ya abiria wa mwaka 2016 waliokuwa 11,868.
Ikumbukwe kuwa kiwanja hicho kilianza kuwa na safari nyingi za ndege baada ya Shirika la ndege la Tanzania (Air Tanzania) kuanzisha rasmi safari zake mkoani humo mapema Januari 2017. Mwaka huo ndiyo pia sehemu ya wafanyakazi wa umma waliokuwa Dar es Salaam walihamishia makazi yao Dodoma kutokana na kampeni ya Rais John Magufuli ya kuhamishia shughuli za Serikali katika jiji hilo.
Hali hiyo pia imewavutia watu wengi zaidi kwenda Dodoma kutafuta fursa za uwekezaji wa biashara ikiwemo maeneo ya kujenga nyumba na majengo ya ofisi.
Hata hivyo, miezi miwili ya Januari na Februari ndiyo ilikuwa na viwango vidogo vya abiria waliotumia uwanja huo ambapo Januari walikuwa 1,035 na kidogo walianza kuongezeka hadi kufikia abiria 1,485.
Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ndiyo ulipokea abiria wengi zaidi mwaka jana waliofikia 2.3 milioni ambapo ni zaidi ya mara 75 ya wale walioutumia uwanja wa ndege wa Dodoma.
Ukuaji huo wa muda mfupi wa uwanja wa ndege wa Dodoma katika sekta ya usafiri wa anga umechochea ,ushindani katika sekta ya usafiri wa anga nchini .
Pia matokeo hayo chanya yamechagizwa na jitihada za makusudi ndani ya Serikali baada ya Serikali kuwekeza katika kufufua Shirika la ndege la Tanzania (Air Tanzania) ambalo hadi sasa lina ndege tano ikiwemo kubwa ya kisasa aina ya Boeing 787-8 Dream Liner.