July 3, 2024

DPP aingilia kati sakata la uhaba wa saruji Tanzania

Aagiza uchunguzi ufanyike juu ya suala hilo kwa sababu kuna viashiria vya utendekaji wa makosa ya jinai yanayohujumu Serikali.

  • Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania amesema amebaini utendekaji wa jinai katika sakata hilo ikiwemo upandishaji bei wa makusudi.
  • Aigiza TAKUKURU na Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai kuchunguza tuhuma hizo.
  • Watakaokutwa na hatia kufungwa jela miaka 20 hadi 30. 

Dar es Salaam. Wakati sakata la uhaba na kupanda bei kwa saruji likiendelea, Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Mganga Biswalo ameagiza uchunguzi ufanyike juu ya suala hilo kwa sababu kuna viashiria vya utendekaji wa makosa ya jinai yanayohujumu Serikali. 

Siku za hivi karibuni, wananchi katika maeneo mbalimbali ya Tanzania wamekuwa wakilalamika kuadimika kwa bidhaa hiyo muhimu ya ujenzi huku baadhi inakopatikana ikiuzwa kwa bei ya juu.

Katika baadhi ya maeneo kumekuwa na ongezeko la bei kati ya Sh3,000 hadi 8,000 kwa mfuko wa kilo 50 kutoka bei ya awali awali ya wastani wa kati ya Sh13,000 na Sh14,000 jijini Dar es Salaam, jambo lililosababisha kupanda kwa gharama za ujenzi.  

Hata hivyo, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa akisema hakuna uhaba wa saruji nchini bali ni watu wachache ambao wameamua kupandisha bei ili kujinufaisha.

Kufuatia hali hiyo, DPP Biswalo leo Novemba 20, 2020 ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi kwa pamoja juu ya tuhuma hizo.

“Nimetoa maelekezo ya kukamilishwa kwa uchunguzi huo katika kipindi cha siku 30 kuanzia 20 Novemba 2020,” amesema DPP.


Soma zaidi: 


Bosi huyo amesema amefikia hatua hiyo baada ya mazingira ya sakata hilo kuashiria utendekaji wa makosa ya jinai katika mnyororo wa uzalishaji, usafirishaji na uuzaji wa saruji kwa wateja, jambo linalosababisha bidhaa hiyo isipatikane kama ilivyo kuwa awali. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa ya mwaka 2019, mtu yeyote aliye au asiye na leseni ya biashara atakuwa ametenda kosa la uhujumu uchumi iwapo atahusika kutengeneza kwa makusudi mazingira yanayoweza kusababisha uhaba na ongezeko la bei ya bidhaa katika soko (Artificial Shortage).

Biswalo amesema baada ya kukamilishwa kwa uchunguzi huo, atachukua hatua stahiki za kisheria kwa watu waliohusika na tuhuma hizo kama anavyoongozwa na ibara ya 59B ya Katiba ya Tanzania ya 1977 na sheria nyingine za nchi.

“Endapo watuhumiwa watafikishwa mahakamani na kutiwa hatiani, wanaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka kati ya 20 hadi 30 gerezani,” amesema Biswalo.