October 6, 2024

Dunia inakabiliwa na uhaba wa vifaa vya kujikinga na virusi vya Corona

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa ulimwengu unakabiliwa na uhaba wa vifaa maalum vya kufunika uso pamoja na vifaa vingine vya kujikinga na virusi vya Corona, jambo linaloweza kuzidi idadi ya vifo vya watu wanaoambukizwa ugonjwa huo.

  • WHO yasema baadhi ya wazalishaji wanatumia janga hilo kama fursa ya kupata faida.
  • Yasema mahitaji ni mengi kuliko vifaa vinavyozalishwa. 
  • Yazitaka Serikali duniani kushikamana na kutanguliza utu kwanza.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO),  Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus ameonya kuwa ulimwengu unakabiliwa na uhaba wa vifaa maalum vya kufunika uso pamoja na vifaa vingine vya kujikinga na virusi vya Corona, jambo linaloweza kuzidi idadi ya vifo vya watu wanaoambukizwa ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa WHO hadi Januari 7 kulikuwa na visa 31,211 vilivyothibitishwa nchini China, na vifo 637 vya maambukizi ya virusi hivyo. Nje ya China, kuna visa 270 katika nchi 24, na kifo kimoja.

Akizungumza jana katika kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa WHO mjini Geneva, Uswisi, Ghebreyesus amesema mapema wiki hii walianza kupeleka vifaa hivyo kwenye nchi zinazohitaji msaada lakini inahitajika matumizi sawa ya vifaa na kuzingatia mizania katika soko katika kukabiliana na virusi vipya vya Corona. 

WHO inakataza uwekaji wa vifaa vya kujikinga katika nchi na maeneo ambamo visa vya maambukizi viko chini,” amesema Dk Ghebreyesus na kuongeza kuwa “wakati idadi ya vifaa ni ndogo na mahitaji ni mengi, basi kuna uwezekano wa watu kuficha vifaa hivyo kwa minajili ya kuviuza kwa bei ya juu.”

Amesema mshikamano unahitajika wakati huu kwa watu kuelewa mapambano dhidi ya virusi vya corona ni nini na kuunga mkono usalama wa binadamu badala ya kutafuta faida. 

“Kwa hivyo kuna suala la maadili hapa pia, na ndiyo sababu tulikuwa na mazungumzo na wazalishaji na wengine pia, ili kushirikiana, na natumai watasimama pamoja kwa msingi wa kuonyesha mshikamano,” amenukuliwa  Dk Ghebreyesus na vyombo vya habari vya kimataifa.


Soma zaidi: 


Ugonjwa huo unasababishwa na kirusi jamii ya Corona na ni kipya “Novel (New) Corona virus 2019” (2019-nCOV) ambacho ni tofauti na virusi vingine vya jamii hiyo ambavyo viliwahi kusababisha milipuko ya ugonjwa uliojulikana kama ‘SARS-CoV’ mwaka 2003 na MERS-CoV Corona Virus mwaka 2013.  

Akinukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa, Mtaalamu wa Programu ya Afya na Dharura wa WHO, Dk Mike Ryan amesema siyo wazalishaji tu, bali wazalishaji wa malighafi, wasambazaji, wauzaji wa jumla wanaweza kupeleka vifaa hivyo kwingine ili kupata faida.

“Kwa hivyo hii siyo shida rahisi kutatua. Kuna wadau wengi, kwa umma na kwenye sekta binafsi. Tunahitaji mshikamano siyo tu kati ya nchi, lakini tunahitaji mshikamano wa kina kati ya umma na sekta binafsi kuhakikisha kuwa hatufiki hatua ambayo wafanyikazi wa afya wanalazimika kuwatunza wagonjwa bila vifaa vya kinga,” amesema Dk Ryan.

WHO imeeleza kuwa kutokana na hatua zinazoendelea kuchukuliwa, katika siku tatu zilizopita pamekuwa na taarifa chache za watu walioambukizwa virusi hivyo nchini China ambayo ni habari njema.

Hata hivyo, imetahadharisha kuhusu kuzitegemea zaidi takwimu zilizopo, kwani idadi ya waathirika inaweza kuongezeka tena.