October 6, 2024

Elimu ya kujikinga na Corona yawafikia wafanyakazi wa nyumbani zaidi ya 200

Elimu hiyo inayohusisha kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuvaa barakoa imetolewa na shirika la kusimamia maslahi ya wafanyakazi wa ndani la WoteSawa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.

Baadhi ya wafanyakazi wa nyumbani wakiwa kwenye banda la maonyesho ya siku ya mfanyakazi wa nyumbani, siku hii huadhimishwa sambamba na siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16. Picha| Mariam John.


  • Ni wa Mkoa wa Mwanza ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo.
  • Elimu hiyo inayohusisha kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuvaa barakoa.
  • Pia wamepatiwa vifaa vitakavyowasaidia kujikinga na ugonjwa huo. 

Mwanza. Zaidi ya wafanyakazi wa nyumbani 200 wamepatiwa elimu ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19 mkoani Mwanza ili kuhakikisha kila kundi kwenye jamii linajumuishwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo. 

Elimu hiyo inayohusisha kunawa mikono, kutumia vitakasa mikono, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuvaa barakoa imetolewa na shirika la kusimamia maslahi ya wafanyakazi wa ndani la WoteSawa kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. 

Mratibu wa Sheria, Utetezi na Uzingatiaji wa shirika hilo, Joseph Mkoji amesema kwa kushirikiana na Serikali mkoani Mwanza wameshiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo kwa kutoa elimu kwa jamii hususani kwa wafanyakazi wa nyumbani.

Wafanyakazi wa nyumbani wako katika hatari zaidi ya kupata maambukizi ya COVID-19 kuliko wafanyakazi walio kwenye ajira rasmi kutokana na mazingira ya kazi zao. 

Hivyo, amesema kuwapatia elimu sahihi ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kunawafanya kuwa sehemu mapambano hayo na kutokuachwa nyuma katika kulinda afya zao. 

Mbali na kutoa elimu hiyo, pia shirika hilo limeweza kutoa ndoo, vitakasa mikono, barakoa kwa wafanyakazi hao kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo wawapo kwenye shughuli zao.

“Wafanyakazi wa nyumbani ni kundi ambalo limesahahulika na kuwa ndiyo kundi ambalo linaongoza kwa kuagizwa kwenda sokoni ambako huko hukutana na watu wa kila aina, bila kumpatia elimu ya namna ya kujikinga anaweza kuwa chanzo cha kueneza ugonjwa huo nyumbani,” amesema Afisa Tathmini na Ufuatiliaji wa shirika la WoteSawa, Masesa Bandoma.

Kutokana na elimu waliyoitoa wameweza kuwafikia wafanyakazi wa nyumbani 200 moja kwa moja kupatiwa na vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa WoteSawa, Angel Benard amesema wanaendelea kuikumbusha Serikali kusaini mkataba wa kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) utakaowasaidia wafanyakazi wa nyumbani kufanya kazi zao katika mazingira mazuri yanayolinda afya zao.

Mkataba huo wa kimataifa uliosainiwa nchini Geneva mwaka 2011 ni daraja kwa wafanyakazi wa nyumbani kupata haki zao za msingi ili waweze kufanya kazi zenye staha.

“Bado kuna changamoto nyingi zinazowakumba wafanyakazi wa nyumbani ikiwemo kubaguliwa, kutengwa, kutokuwa na mikataba ya ajira, hivyo kusainiwa kwa mkataba huo kutapunguza changamoto hii na kumsaidia mfanyakazi wa nyumbani kujiamini,” amesema Benard.