October 6, 2024

Epuka haya wakati unaanzisha biashara

Mambo ya kuepuka ni pamoja na kujiwekea matumaini makubwa na kufanya kazi peke yako.

  • Mambo ya kuepuka ni pamoja na kujiwekea matumaini makubwa na kufanya kazi peke yako.
  • Usibweteke na mafanikio ya muda mfupi. 

Huenda umepata elimu ya ujasiriamali na umeambiwa mambo mengi unayotakiwa kufanya kabla ya kuanzisha biashara ili ufanikiwe katika safari yako ya kujiajiri. 

Elimu ya sahihi ya kuanzisha biashara lazima iambatane na kuambiwa mambo ambayo unatakiwa kuyaepuka kabisa katika shughuli zako. Kama kweli unakusudia kuingia katika biashara basi epuka mambo haya:

 Achana na kuwaza kufanikiwa tu

Kila mjasiriamali ana ndoto kubwa ya kufanikiwa lakini wakati mwingine mambo yanaenda tofauti. Utakutana na yasiyotarajiwa na uwe tayari kukabiliana nayo. Kuna kushindwa na kukatishwa tamaa. 

Wakati unaanzisha biashara, uwe na mpango wa dharura utakaokuinua pale mambo yanapoenda sivyo ikiwemo akiba ya fedha ili kuhakikisha unaendelea kuwepo kwenye soko la ushindani na kutengeneza faida.


Soma zaidi:


Kufanya yote peke yako

Kuwa na watu wenye ujuzi tofauti katika biashara yako kunajenga msingi imara wa  kuaminiwa na kuepuka makosa yasiyo ya lazima. Usijifanye unajua kila kitu, wape fursa watu  wenye ujuzi na maarifa katika biashara kukushauri na hata kufanya shughuli zingine ambazo zinahitaji utaalam. 

Biashara ni watu, ukifanya peke yako hutafanikiwa, utaelemewa na majukumu na ufanisi utapungua. Gawa majukumu kwa wengine. Lakini hili linategemea na aina ya biashara unayotaka kufanya. 

Kufanya kazi na marafiki

Epuka kuendesha biashara kwa mtindo wa urafiki uliosoma nao au ndugu unaowajua. Tafuta wabia wenye weledi watakaokusaidia kuikuza biashara yako. 

Biashara ni kazi inayopaswa kukuingizia kipato, weka kando urafiki kwenye shughuli zako rasmi.

Epuka mahusiano yako na marafiki kuingilia shughuli za biashara yako. Picha|K15 Photos. 

Kushangilia mafanikio ya muda mfupi

Kuna wakati biashara yako inaweza kustawi sana na ukajikuta umepata mafanikio kwa muda mfupi yaani kila kitu kinaenda sawa. Huo ndiyo wakati wa kutafakari na siyo kubwetekwa. 

Mafanikio yakupe uwezo wa kujiimarisha zaidi na kuhakikisha huduma na bidhaa zinatolewa vizuri, huku ukiwekeza kutafuta masoko mapya ili kutekeleza mipango ya muda mrefu. 

Usikubali mafanikio ya muda mfupi yakuzuie kufikia ndoto za maisha yako. Furahia lakini kwa tahadhari ukijua unaweza kuanguka usipokua makini. 

Kuendesha biashara bila usajili

Biashara zinaendeshwa kwa namna mbalimbali, lakini leseni ya biashara kutoka mamlaka husika za Serikali ni muhimu kwa sababu kila jambo linaendeshwa kwa matakwa ya sheria. Epuka ‘ujanja ujanja’ wakati unaendesha shughuli zako. 

Biashara inayotambulika kisheria inaaminiwa zaidi na wateja wako na ni rahisi kupewa miradi ya kufanya ili uongeze kipato.