July 3, 2024

Epuka uzushi wa kipimo kipya cha Corona kilichotangazwa na China

Ni kile cha haja kubwa kilichotangazwa na China hivi karibuni.

  • Ni kile cha haja kubwa kilichotangazwa na China hivi karibuni.
  • Baadhi ya wazushi wasema ni kikubwa kuliko maumbile ya mwanadamu. 
  • China haijatangaza kama kitatumika katika maeneo mengine duniani.

Dar es Salaam. Kipimo kipya cha ugonjwa wa Corona kwa kutumia njia ya haja kubwa kilichotangazwa hivi karibuni na China, kimeendelea kuzua gumzo mtandaoni kwa watu kutoa maoni tofauti kuhusu matumizi yake. 

Lakini mijadala hiyo imeenda mbali kwa baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kutengeneza habari za uzushi kwa kuweka picha zisizo halisi zinazodhaniwa ni za kipimo hicho.

 Moja ya picha inayosambaa mtandaoni hasa Facebook ni inayomuonyesha mwanaume akiwa amesimama huku akiwa amaeshikilia fimbo ndefu inayofanana na vifaa vya kusafishia masikio kwa kutumia pamba. 

Wanaosambaza picha hiyo wanadai kuwa hicho ndiyo kipimo kipya cha haja kubwa kitakachotumiwa kuwapima wagonjwa wa Corona. Hata hivyo, picha hizo siyo za kweli ni uzushi. 


Mashaka yaliyopo kwenye hiyo picha  

Kwanza ni ukubwa wa kifaa hicho. Hiyo inalenga kuwaogopesha watu kuhusu Corona kwa sababu hakuna kipimo cha Corona chenye ukubwa wa namna hiyo. 

Vipimo vya Corona ikijumuisha vile vya kuingiza puani na mdomoni ni vidogo na vinaendana na maumbile ya binadamu. 

Pia Nukta Fakti imetumia zana za kidijitali ikiwemo Google Image Reverse na TinEye na imebaini kuwa picha hiyo haina uhusiano wowote na kipimo kipya kilichogunduliwa na China na haijatumika katika matukio mengine zaidi ya hilo la uzushi. 

Huenda picha hiyo imehaririwa na kuongezewa baadhi ya vitu ili ifanane na kifaa chenye pamba kinachotumika kusafishia masikio na watu waliotengeneza kukihusisha na kipimo kipya cha Corona.  


Zinazohusiana:


Kwa mujibu taarifa za China za kipimo hicho (Anal Swab) kinatumika kwa makundi maalum yaliyoteuliwa ya watu hasa watu waliopo karantini na wenye uwezekano mkubwa wa kupata maambukizi ya Corona nchi humo. 

Tovuti ya masuala ya afya ya WebMD imeeleza kuwa kipimo hicho kina urefu nchi moja hadi mbili tofauti na inavyoripotiwa na baadhi ya watu mtandaoni. 

Hata hivyo, China haijaeleza kwa undani kama kipimo hicho kitatumika katika mataifa mengine kama ambavyo imekuwa ikienezwa na baadhi ya watu kwa lengo la kuwatisha na kutaka wasikubali kukitumia. 

Ni muhimu kupata taarifa sahihi kuhusu vipimo vya Corona kutoka mamlaka za afya ikiwemo Wizara ya Afya ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kuepuka madhara ya habari za uzushi.