Facebook yaendeleza vita ya Corona kupitia makundi
Mtandao wa Facebook umetangaza ratiba ya mafunzo maalum kwa viongozi wa makundi ya mtandao huo yatakayowasaidia kuongoza vema jamii za watu katika makundi yao na kuongeza wigo wa kupambana na habari za uzushi
- Itaanza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo viongozi wa makundi namna ya kuwaongoza watu.
- Pia mafunzo hayo yanalenga kupambana na habari za uzushi kuhusu Corona.
Dar es Salaam. Mtandao wa Facebook umetangaza ratiba ya mafunzo maalum kwa viongozi wa makundi ya mtandao huo yatakayowasaidia kuongoza vema jamii za watu katika makundi yao na kuongeza wigo wa kupambana na habari za uzushi kuhusu mada mbalimbali ikiwemo virusi vya Corona (COVID-19).
Mafunzo hayo ni mfululizo wa warsha za mtandaoni zinazofanywa na Facebook kuwasaidia watumiaji wake kuwa salama na kuendeleza ushirikiano dhidi ya COVID-19.
Mafunzo hayo yanayofanyika kila mwezi yatawajengea uwezo viongozi wa kusimamia vizuri watu katika makundi yao na kuhakikisha wanakuwa salama dhidi ya hatari yoyote ikiwemo uzushi kuhusu COVID-19.
Mathalan, mwezi huu wa Mei mada itakayoongelewa katika mafunzo hayo itakuwa misingi ya kusimamia makundi huku Juni watajikita katika kuangalia mambo yatakayosaidia ukuaji wa makundi na kupata watu sahihi wenye uwezo kuendeleza mijadala yenye maslahi mapana kwa watu.
Mafunzo hayo yatatolewa na wataalam wa mitandao ya kijamii ikiwemo mwanzilishi wa mtandao huo, Mark Zuckerberg ambaye atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Facebook inawaunganisha zaidi watu kipindi hiki cha mlipuko wa Corona.
Makundi ya mtandao huo yamekuwa nyenzo muhimu ya watu kukutana na kubadilishana mawazo ikizingatiwa kuwa kwa sasa watu wengi hawawezi kuonana kutokana na athari za Corona.
Zinazohusiana:
- Facebook kuanza kuwachaguliwa wafuasi wake viongozi wa makundi
- Facebook yabuni mfumo mpya wa kupambana na matapeli mtandaoni
Facebook imeeleza kuwa watumiaji zaidi ya bilioni 1.4 wanatumia makundi ya mtandao huo kila mwezi huku watumiaji milioni 200 wakiwa ni wanachama hai wa makundi hayo.
Hata hivyo, ongezeko la watumiaji wa makundi hayo limechochewa na COVID-19 ambapo watu wanatafuta taarifa sahihi na kujua nini kinaendelea duniani kuhusu ugonjwa huo.
Kutokana na ongezeko hilo, Facebook imelazimika kutoa mafunzo kwa viongozi wa makundi ili kuwapatia zana na mbinu zitazosaidia kukabiliana na habari za uzushi wakati wa mijadala yao.
Mtumiaji wa mtandao huo, Hellen Maumba wa jijini Dar es Salaam amesema hatua hiyo ya Facebook ina maana kwa sababu makundi mengi ya mtandao huo yamekosa mwelekeo licha ya kuwa na malengo mazuri wakati wa kuyaunda.
“Itasaidia hasa sisi ambao tunaingia kwenye makundi hayo ili tujielimishe zaidi kwa mambo mbalimbali lakini wakati mwingine tunajitoa kwa sababu yanakosa mvuto na mwelekeo,” amesema Maumba.
Mafunzo hayo yatakuwa yanatolewa katika ukurasa rasmi wa Facebook Community ambapo watu wengine wasio viongozi wa makundi wanaweza kushiriki.