October 6, 2024

Fahamu njia 3 kuongeza kipato cha familia

Ainisha mipango ya muda mfupi na muda mrefu ili kufahamu kiasi cha pesa kinachohitajika katika utekelezaji wake.

  • Ainisha mipango ya muda mfupi na muda mrefu ili kufahamu kiasi cha pesa kinachohitajika katika utekelezaji wake.
  • Weka akiba kwa kila mapato unayoyapata ili ikusaidie wakati wa dharura.
  • Kuwa mbunifu wa vyanzo vipya vya mapato na kubali mabadiliko ya tabia ya matumizi ya pesa.

Kuweka akiba ya fedha kwa matumizi binafsi inaweza isiwe jambo rahisi kwa watu wengi, lakini ni zaidi sana ukiwa na familia kutokana na majukumu unayopaswa uyakamilishe ili maisha yaendelee. 

Kuweka akiba au kutunza fedha kwa matumizi ya baadaye ni sehemu ya maendeleo na kukusitiri wakati wa dharura zinazoweza kujitokeza wakati wowote.

Zipo njia rahisi unazoweza kuzitumia kukusaidia kuweka akiba wakati ukitimiza malengo ya muda mfupi na muda mrefu yanayohusu familia yako. 

Anzisha mfuko wa dharura

Huwezi kujua yatakayotokea baada ya siku moja ya kuishi kwako. Mtoto wako anaweza akaugua au mwanafamilia akapata ajali. Hata hivyo hatuombei yatokee lakini kuna umuhimu wa kutunza pesa kwa ajili ua dharura. 

Akiba hata ikiwa kidogo kiasi gani inaweza kuleta matokeo pale itakapohitajika.


Soma zaidi: bajeti inavyookoa matumizi mabaya ya pesa ngazi ya familia


Angalia zaidi vipaumbele vya muda mrefu

Watalaam wa mipango wanashauri kuwa katika mipango yako ya muda mrefu, weka kipaumbele cha akiba ya uzeeni, hata ada ya watoto wako ambao wanategemea kujiunga na chuo kikuu. 

Mipango pia inaweza kuwa kujenga nyumba na kuachana na kusihi katika nyumba za kupanga. Kwa kijana mwenye wazazi wenye umri mkubwa pia unapaswa jinsi ya kufikiri kuwasaidia kwa kuanza kuwawekea akiba itakayowasaidia uzeeni wakati hawana nguvu ya kufanya kazi. 

Mipango ya mapato na matumizi inasaidia kujua ni kiasi cha pesa kinachoelekezwa kwenye kibubu cha akiba kwa ajili ya malengo ya familia. Picha|pulse.ng

Usisahau malengo ya muda mfupi. 

Kama umejiridhisha kuwa una uhakika wa akiba ya kukamilisha malengo ya muda mrefu, unaweza kugeukia malengo ya muda mrefu ambayo unaweza kuyakamilisha taratibu bila kusahau mahitaji ya kila ya famili.

Unaweza kufungua akaunti ya benki au simu benki kwa ajili ya kila lengo kubwa unalotaka kukamilisha. Weka akiba kila wiki au mwezi kulingana na upatikanaji na ukubwa wa mfuko wako. 

Kumbuka akiba ni muhimu lakini mahitaji ya kila siku ya familia ikiwemo upatikanaji wa chakula bora ni muhimu zaidi kukuhakikishia afya bora ya kutafuta pesa. Picha|blackenterprise.com

Kuwa mbunifu na kubali mabadiliko

Akiba hutegemea uwezo wako wa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato.Kama ni mfanyakazi tafuta biashara ya kufanya ambayo itasaidia kuongeza kipato cha familia na kupata fedha za kufikia malengo yako. 

Lakini unapaswa kubadilika kitabia juu ya matumizi ya pesa zako. Punguza matumizi yasiyo ya lazima na tumia pesa kwenye mambo ya msingi kwa lugha nyingine funga mkanda. Mambo yote haya hayawezekani kama huna mipango endelevu ya maisha na familia yako. 

Hata hivyo, ukweli utabaki kuwa kuweka akiba ni maumivu lakini ukivumilia utayaona matunda yake.