July 5, 2024

Fahamu undani wa chanjo ya Corona ya Janssen

Ni chanjo inayotengenezwa Marekani na hutolewa dozi moja tu kwa mtu anayepatiwa.

  • Ni chanjo aina ya Johnson & Johnson inayotengenezwa Marekani.
  • Mtu anayepewa chanjo hii anatakiwa kupata dozi tu.
  • Pia inawafaa watu wenye magonjwa sugu kama kisukari.

Dar es Salaam. Mpaka sasa, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeidhinisha matumizi ya chanjo sita dhidi ya ugonjwa Corona ikiwemo Janssen ambayo inawezakutumika kwa matumizi ya dharura pia inaweza kutumika kwa kwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.

Pia chanjo hiyo inawafaa watu wenye magonjwa sugu ikiwemo kisukari,

Chanjo nyingine ni Pfizer/BioNTech, AstraZeneca/Oxford, Moderna,Sinovac na Sinopharm. Chanjo hizo nia zingine zaidi ya 200 ambazo ziko kwenye utafiti zitatumika kuikabili Corona ambayo inaitesa dunia kwa sasa.

Mtumiaji wa chanjo ya Janssen maarufu kwa jina la Johnson & Johnson anatakiwa kupatiwa dozi mmoja ya chanjo (0.5) ambapo ni tofauti na chanjo nyingine kama AstraZeneca/Oxford ambazo mtu anapatiwa dozi mbili.

Mtu anayepewa chanjo hii anatakiwa kupata dozi moja tu. Picha| Getty Image.

Chanjo hiyo inafaa wa kina nani?

Chanjo ya Janssen ambayo imetengenezwa Marekani imependekezwa kutumiwa na wafanyakazi ambao maisha yao yapo hatarini kutokana na kazi zao sambamba na watu wazima.

Pia chanjo hiyo ambayo inatumiwa na nchi za Ulaya, Afrika na Amerika inaweza kutolewa kwa watu wenye shinikizo la damu, ugonjwa sugu wa mapafu, ugonjwa wenye virusi vya Ukimwi na kisukari.

Wakina mama wanaonyonyesha na wajawazito nao wanaweza kupatiwa baada ya kupata ushauri wa daktari kuwa italeta matokeo mazuri, imeeleza WHO katika taarifa yake kuhusu chanjo hiyo.

Hata hivyo, mtu yeyote ambaye ana joto zaidi ya nyuzijoto 38.5 hatatakiwa kuchanjwa hadi joto litakapo shuka. Vilevile chanjo haishauriwi kutolewa kwa watu walio chini ya miaka 18.

Chanjo ni silaha muhimu wakati huu kuikabili Corona kwa sababu inatoa uhakika mkubwa wa kumkinga mtu endapo atapatiwa.