November 24, 2024

Faida za kusoma tabia ya mteja wako katika biashara

Unakusaidia kupanga bei na kutokufanya makosa ambayo watoa huduma waliopo wanayafanya.

  • Ni pamoja na kufahamu mahitaji sahihi ya wateja wako.
  • Unakusaidia kupanga bei na kutokufanya makosa ambayo watoa huduma waliopo wanayafanya.
  • Kutakufanya kupata ubunifu wa kuwavutia wateja wako kwa urahisi.

Dar es Salaam. Chukulia mfano umefungua mgahawa wa kuuza chakula karibu na ofisi za wafanyakazi wa shirika au kampuni fulani. Huwezi kuwapata watu hao na kuwafanya wateja wako kwa kuwaunga kamba na kuwavuta mgahawani kwako.

Utahitaji kufanya utafiti kufahamu tabia zao na kufahamu wanahitaji au wanakosa nini kutoka kwa mtu anayewahudumia. 

Kupitia utafiti na kusoma tabia za watu wanaoweza kuwa wateja wako, unaweza kuwa bora na kuwapata wateja hao na hivyo kuingia katika ushindani kati yako na mtoa huduma ambaye alikuwepo awali.

Zifuatazo ni faida za kusoma au kutafiti tabia za wateja pale unapoanzisha biashara:

Kufanya utafiti kutakutambulisha vyema sokoni

Kuwa na bidhaa au huduma bora kuliko watu wote uliowakuta sokoni  haitoshi kuwafanya wateja wafurike kwenye biashara yako.

Kwa baadhi ya wateja wanavutiwa na huduma nzuri kwa wateja, usafi na wengine na ubora wa bidhaa. Hivyo kwa kufanya utafiti, itakusaidia kufahamu uitambulishaje bidhaa au huduma yako kwa watu wanaofaa kuwa wateja wako.

Kwa baadhi huenda mbali na kutenga siku maalumu ya uzinduzi wa biashara ambayo hutoa mialiko kwa watu wanaoona wanaweza kuwa wateja wao na kisha kutambulisha bidhaa/ huduma zao.

Utafiti utakusaidia kupanga bei, kufahamu mahitaji ya wateja wako na kuelewa makosa ya watangulizi wako. Picha| Dreamstime.com. 

Itakusaidia katika kupanga bei ya bidhaa au huduma yako

Unaweza kuanzisha mgahawa au bidhaa ambayo ina ubora wa hali ya  juu katika eneo fulani lakini kitu ambacho umeshindwa kufikiri ni tabia za manunuzi za watu wanaozunguka eneo lako kama wanaweza kuendana na bei hiyo.

Wateja wengine huishi ndani ya bajeti ya kipato chao na hivyo kupandisha kiwango cha matumizi yao kwa siku inaweza kuwa changamoto kununua bidhaa zako.

Kabla ya kuanzisha huduma au bidhaa yako, inashauriwa kusoma tabia ya matumizi ya mteja wako kwa kuona wapi hupata huduma zake na kwa kiasi gani cha fedha. Itamvutia kupata nguvu ya kujaribu bidhaa zako kwani anafahamu kuwa anaweza kuzimudu.

Kufahamu mambo wanayopenda wateja wako

Unapoanza biashara unahitaji kuwa tofauti na watoa huduma uliowakuta lakini je, wenyeji wa hapo wanahitaji kitu kipya au tayari wamefungamana na huduma zilizopo?

Mfano, unaweza kukuta sehemu kuna migahawa mingi ya chipsi ukaamua uanze kupika makande. Je wateja wa hapo watahitaji makande kwa kiwango cha kukupatia faida?

Endapo utafanya utafiti, itakusaidia kufahamu bidhaa gani wanaihitaji au huduma ipi wanahitaji iboreshwe.


Soma zaidi:


Utafahamu muda sahihi wa kutoa huduma yako

Unaweza kushangaa kuwa zipo biashara ambazo wenye biashara hufungua saa tano za asubuhi, wengine wanafungua saa kumi na mbili asubuhi huku wengine wakianza kazi mchana kabisa. 

Wote hao siyo kuwa hawafahamu wanalolifanya, wamefanya utafiti kwa wateja wao.

Kabla ya kuanza biashara, hakikisha unafahamu muda ambao wateja wako wataanza kuihitaji huduma yako. Mfano, kwa ofisi nyingi, muda wa chakula ni saa saba mchana, hivyo wewe kuivisha chakula saa tisa, huenda ukakosa wateja wengi sana mgahawani mwako.

Lakini ukifahamu muda ambao huduma yako inaanza kuhitajika na wateja, hautoamka saa nne asubuhi kuanza kukaanga mihogo kwa ajili ya watu kunywa chai au kufungua biashara ya kuuza maji katika kipindi cha mvua katika jamii ya watu waliojenga matenki ya kuvuna maji ya mvua.

Kwa upande wako unafikiri umuhimu mwingine wa utafiti wa wateja kabla ya kuanza biashara ni upi? Tuandikie maoni yako kupitia @NuktaTanzania katika mitandao ya kijamii ya Twitter, Instagram na Facebook.