Fanya haya kabla ya kukata katika biashara yako
Tafuta furaha ambayo ulikuwa nayo mwanzoni wakati unaanzisha biashara ua kampuni yako.
- Tafuta furaha ambayo ulikuwa nayo mwanzoni wakati unaanzisha biashara ua kampuni yako.
- Ongea na wenzako. Iwe timu au wafanyakazi wako, hakikisha wako sawa.
- Endapo unahisi umezidiwa majukumu,tafuta msaidizi.
Kukata tamaa ni jambo jepesi hasa pale mtu unapoona mambo yako hayaendi na mipango yako inagoma kila ukiipanga. Unaweza kuhisi kuwa ni mkosi, kuna sehemu unakosea na kwa baadhi, hudhani ni laana kutoka kwa wahenga wao.
Katika maisha inashauriwa kutokufanya hivyo kwa sababu wengine huwa karibu katika kupata mafanikio yao wakati wanapoanza kukata tamaa na kukosa walichokusudia.
Moja ya rafiki zangu aliwahi kuniambia, “unapokata tamaa hakikisha ulikuwa umewekeza kila tone la juhudi zako na haukufanikiwa”
Lakini vipo baadhi ya viashiria vinavyoweza kujitokeza wakati ukiendelea na shughuli za kikazi au biashara ambavyo vinaweza kuwa sababu ya wewe kukata tamaa katika kile unachokifanya.
“Unapokata tamaa hakikisha ulikuwa umewekeza kila tone la juhudi zako na haukufanikiwa”. Picha| Freepik
Dalili hizi ni kiashiria tosha kuwa umeanza kukata tamaa katika kile unachokifanya:
Endapo hauna furaha kama uliyokuwa nayo mwanzo
Kwa ndoto ambayo unaipambania, ni lazima ufurahie mchakato wa upambanaji kwani kuna siku utachelewa kulala, siku unaweza kupiga pasi ndefu na siku zingine unaweza utoboe usiku mzima ukipambania ndoto zako.
Kwa mtu ambaye anapenda anachokifanya, hawezi kuona hiyo kama changamoto kwake bali mchakato wa kufikia malengo yake. Hata hivyo inapofika mahali hauna furaha tena na unachokifanya kiasi cha kuona uvivu kuamka kwenda kufanya kazi zako, hiyo ni bendera nyekundu.
Ni kiashiria kuwa kuna kitu hakipo sawa na unahitaji kurekebisha. Inaweza kuwa haupati muda wa kupumzika vizuri au unahitaji kupitia upya mipango yako uliyonayo kwani iliyopo huenda haifanyi kazi.
Unaweza kuchukua likizo ili upate muda wa kupumzika na kufanya mipango yako vizuri ili urudi katika hali ya kawaida.
Hauridhishwi na utendaji kazi wa wafanyakazi wako
Kwa kazi ambazo zinafanyika katika timu, inahitaji wewe na timu yako wote muwe katika ukurasa mmoja.
Pale wenzako wanapokuwa hawana furaha na kazi zao, ni kiashiria kuwa mambo hayapo sawa na itakuchelewesha kufikia malengo yako na ya kampuni yako kwa ujumla.
Endapo hali iko hivyo, unashauriwa kuongea na timu yako, kuwekana sawa na kusikiliza sababu zinazofanya washindwe kuendana na kasi yako.
Unaweza kuchukua likizo ili upate muda wa kupumzika na kufanya mipango yako vizuri ili urudi katika hali ya kawaida. Picha| Freepik.
Unapohisi unazidiwa kimajukumu
Kuongezeka majukumu ni kiashiria kizuri ya kuwa biashara yako au kampuni yako inakua na pia una kazi za kufanya.
Lakini pale majukumu yanapokuwa mengi kuliko uwezo wako, ni kiashiria kuwa umezidiwa na huenda ukashindwa kuridhisha baadhi ya wateja wanaohitaji huduma yako.
Mfano, kama wewe unatoa huduma ya chakula, pale unapokuwa na wateja wengi katika mgahawa wako kiasi cha kushindwa kuwahudumia ipasavyo, ni dalili ya kuwa umezidiwa na unahitaji kuongeza timu yako ili msaidiane kufikia lengo.
Inashauriwa kuongeza timu yako au kutafuta msaidizi wa kukusaidia kazi ambazo unashindwa kuzifanya.