November 24, 2024

FinSights Lab yapania kuboresha maisha ya wafanyabiashara Tanzania

Ni chombo muhimu katika kuibua mbinu mpya za kukabiliana na ushindani wa soko na huduma za kifedha.

  • Itawahusu zaidi wafanyabiashara wanaochipukia, mashirika, wabunifu wenye ndoto za kuboresha biashara zao.
  • Ni chombo muhimu katika kuibua mbinu mpya za kukabiliana na ushindani wa soko na huduma za kifedha.

Dar es Salaam. Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) umefungua milango kwa wafanyabiashara wenye nia ya kukuza biashara zao kujiunga katika mafunzo yanayotolewa na kituo atamizi cha FinSights Lab ili kutatua changamoto za masoko na huduma za fedha katika shughuli zao.

FinSights Lab ni muendelezo wa juhudi mbalimbali za wadau wa teknolojia hapa nchini kutafuta njia rahisi za kutatua changamoto za kijamii na kuinua maisha ya watanzania wenye mawazo na miradi ya kibunifu.

Atamizi hiyo inalenga kupunguza changamoto  katika uendeshaji wa mashirika binafsi na  ya umma katika sekta ya fedha na kuongeza wigo wa utoaji huduma na upatikanaji wa masoko kwa ajili ya biashara. 

Kwa mujibu wa taarifa ya FSDT iliyotolewa kwa umma, mfumo wa utendaji wa atamizi hiyo ni kutoa jukwaa huru kwa wataalam waliobobea katika masuala ya tabia, sayansi ya takwimu wenye ujuzi na uzoefu wa kufanya tafiti mbalimbali kukaa pamoja na wafanyabiashara wanaochipukia  kuchanganua tatizo, kubuni suluhisho, kujaribu ubora wa suluhisho na kupanga njia sahihi ya kupata matokeo yanayokusudiwa.

“FinSights imetenengenezwa kutoa suluhisho katika mazingira mbalimbali, kwa kuleta ujuzi huu kwenye soko itasaidia kuibua ubunifu unaohitajika kwenye huduma za fedha Tanzania,” anaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia kupitia mafunzo hayo, yatasaidia kufahamu sera na miongozo ya biashara nchini ambapo thamani ya wazo au bidhaa ya mtu atawekewa mazingira ya kuboreshwa ili ikubalike kwenye soko la ushindani.


Zinazohusiana:


Muitikio wa watu hasa vijana kuanzisha biashara na kampuni umekuwa mkubwa lakini changamoto inayojitokeza ni ukosefu wa ujuzi na maarifa ya kuendeleza biashara hizo na uwezo mdogo wa kusimamia mwenendo mapato. 

Mfuko waFSDT ni taasisi inayolengo la kuimarisha mfumo wa soko ambao unawanufaisha watu, kaya na wajasiriamali kwa kuwajengea uwezo na kuwapa fursa ili kuboresha maisha yao. Hii inajumuisha kubainisha changamoto na kusaidia ubunifu na kujenga uhusiano katika sekta ya fedha kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali katika sekta hiyo.