July 8, 2024

Fursa zinazoweza kuwatoa kimaisha Watanzania Uchaguzi Mkuu 2020

Zipo fursa za kibiashara ambazo watu wanaweza kuangazia zikiwemo uuzaji wa chakula, huduma za malazi na usafiri.

  • Ni pamoja na kushiriki kwenye kampeni zenyewe ili kujuana na watu pamoja na wagombea.
  • Zipo pia fursa za kibiashara ambazo watu wanaweza kuangazia zikiwemo uuzaji wa chakula, huduma za malazi na usafiri.
  • Kwa wale wenye vipaji, wanaweza kutumia vipaji vyao ikiwemo kuimba na kuchora. 

Dar es Salaam. Ni wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu Tanzania, ambao unatoa fursa kwa Watanzania kusikiliza sera za wagombea wa vyama vya siasa kabla ya kuwapigia kura Oktoba 28, 2020.

Uchaguzi huo unaofanyika kila baada ya miaka mitano, siyo kwa ajili ya wanasiasa kunadi sera kwa wapiga kura, lakini ni kipindi muhimu ambacho kina fursa mbalimbali ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwatoa kimaisha Watanzania. 

Bado hujaziona? Fungua macho yako, uchaguzi wa mwaka huu una fursa lukuki ambazo zinaweza kukuingizia kipato na hata kuongeza wigo wa mtandao wa marafiki na wafanyabiashara. Fursa hizo ni zipi?

Kushiriki kwenye kampeni

Mwakilishi wa vijana nchi za Jumuiya ya Madola Badru Rajabu amesema vijana wanaweza wasiione hiyo kama fursa lakini ni kipindi muhimu kwa watu wenye malengo ya muda mrefu ya kujenga mtandao na mahusiano mazuri kwenye jamii. 

Kupitia kushiriki kwenye kampeni, mtu anaweza kuuza kile anachokifanya na akakutana na watu mbalimbali wa kubadilishana uzoefu wa utendaji wa shughuli zake. 

“Ni muda wa kuanza kuchangamana hata na wagombea. Huwezi kujua mbeleni itakuaje,” amesema Rajabu.

Unapohudhuria kampeni, unaweza kukutana na marafiki wapya na hata kutengeneza mahusiano chanya na wagombea. Picha| Jamii Forums.

Uhamasishaji na uraghabishi

Kwa vijana wanaopenda kujitolea katika shughuli za kijamii, huu ndiyo muda wake kwa sababu wanaweza kuutumia kutoa hamasa kwa wapiga kura kushiriki kikamilifu katika kampeni zinazoendelea maeneo mbalimbali kabla ya kupiga kura Oktoba 28. 

Hatua hiyo itakuongezea uzoefu wa kufanya kazi na jamii na uchambuzi wa masuala muhimu yanayogusa maisha ya watu kwa sababu utapata fursa ya kusoma ilani za vyama vya siasa na kupata maoni ya wananchi. 

Fursa za kibiashara

Kuna fursa nyingi za kibiashara katika kipindi hiki cha kampeni za Uchaguzi Mkuu zikiwemo kuuza chakula, kukodisha vyombo vya usafiri na muziki, usafiri, mahema, kutoa huduma za malazi, kutengeneza matangazo na vipeperushi. Ni nyingi kuzitaja. 

Angalia ni ipi inakufaa na wafuate wanasiasa ambao ndiyo wadau muhimu. 

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Ramadhan Mgeni aliyetarajia kwenda Mkoa waShinyanga hivi karibuni amejikuta akikosa hoteli alizokuwa akizihitaji kutumia akifika mkoani humo kwa sababu wanasiasa wamezichukua tayari.

“Nina safiri Ijumaa na nilikuwa natafuta hoteli tangu Jumatatu (Septemba 7, 2020), nimekosa naambiwa zimejaa shauri ya kampeni,” ameeleza Mgeni.


Soma Zaidi


Fursa zinazoendana na talanta za watu

Katika kipindi cha kampeni, wagombea wengi hujitahidi kuibuka na namna za tofauti za kufanikisha na kuvutia mikusanyiko.

Mbali na vitenge na khanga ama tisheti, wengine wameanza kutumia muziki, maigizo na hata vipeperushi kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi.

Hapo ndipo watu wenye vipaji wanapotakiwa kukuna vichwa wakikamatia fursa hizo.

Mbunifu na mtaalam wa masuala ya picha, Evon Evance ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa vijana wanatakiwa kutafuta fursa hizi kwa sababu ni kipindi sahihi kunoa vipaji vyao.

“Katika kipindi hiki vijana wana nafasi kubwa sana. Hasa katika masuala ya mtandao na ubunifu. Wagombea wengi wanajitahidi kuwafikia vijana na ni vijana ndio wanaoweza kulifanikisha hilo kwani wanajua kile vijana wenzao wanahitaji,” amesema Evance.

Msanii Diamond Platnumuz akitumbuiza katika moja ya mikutano ya CCM mwaka huu. Picha| CCM

Zaidi, binti huyo amesema mbali na fursa za vipaji, zipo fursa za teknolojia kama uratibu wa mitandao ya kijamii au tovuti za wagombea na vyama vya siasa. 

“Badala ya kutegemea kampeni za ana kwa ana katika kipindi hiki ambacho watu wana mambo mengi, vijana wanaweza kuwashauri wagombea kuangazia mitandao ya kijamii na tovuti katika kampeni zao,” ameelezea Evance ambaye fursa za uchaguzi hazijampita.

Bado hujachelewa, kampeni zinaendelea katika maeneo mbalimbali Tanzania, tafuta fursa inayokufaa, itumie na boresha maisha yako.