November 24, 2024

Gavana Florens Luoga hajafungua akaunti Facebook-BoT

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema Gavana wa benki hiyo, Profesa Florens Luoga hajafungua akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook, kinyume na taarifa na picha zinazojitokeza katika mtandao huo kwa jina lake.

  • Imesema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga hajafungua akaunti ya Facebook, kinyume na taarifa na picha zinazojitokeza katika mtandao huo kwa jina lake.
  • Watanzania watakiwa kupuuza taarifa yoyote inayotolewa na akaunti hiyo bandia inayojiita Frolence Luoga.
  • BoT imeeleza kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa ili kumbaini mhalifu aliyefungua akaunti hiyo.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema Gavana wa benki hiyo, Profesa Florens Luoga hajafungua akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook, kinyume na taarifa na picha zinazojitokeza katika mtandao huo kwa jina lake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Oktoba 29,2019)  na Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki ya BoT imeutaka umma wa Watanzania kupuuza taarifa yoyote inayotolewa na akaunti hiyo bandia inayojiita Frolence Luoga na ambayo inatumia picha mbalimbali za Gavana wa BoT kinyume na sheria,

“Tunauhakikishia umma kwamba, Gavana Luoga hajafungua akaunti kwa jina hilo na hivyo taarifa zozote zitakazotolewa kwenye akaunti hiyo ya Facebook hazina uhusiano wowote na Prof. Florens Luoga,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo inayopatikana katika ukurasa wa Twitter wa BoT.

Hata hivyo, BoT imeeleza kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa ili kumbaini mhalifu huyo kwa kutumia akaunti hiyo kuchafua sifa ya  Gavana Luoga kwenye jamii. 

Taarifa hiyo haijaeleza kwa undani ni kwa namna gani akaunti hiyo imechafua sifa ya Prof Luoga.