November 24, 2024

Gharama utakazolipa unapoamua kujichubua ngozi-2

Madhara ya kujichubua huwatumbukiza wahusika kwenye umaskini wa kipato ambao siyo rahisi kutoka.

  • Bidhaa za kujichubua huingiza sumu mwilini na kusababisha magonjwa yakiwemo ya figo.
  • Mbali na maradhi, ngozi hujikunja na kumfanya mtu kuzeeka mapema.
  • Madhara ya kujichubua huwatumbukiza wahusika kwenye umaskini wa kipato.

Dar es Salaam. Katika makala iliyopita tuliangazia viambata na kemikali zilizopo kwenye vipodozi vinavyoharibu mfumo wa ngozi. Leo tena tunaangazia madhara ya kujichubua na jinsi mtu aliyeathirika anavyoweza kurejea katika hali ya kawaida. 

Kimsingi, bidhaa za kujichubua huingiza  sumu mwilini na hivyo kusababisha changamoto mbalimbali za kiafya ikiwemo magonjwa ya figo na saratani.

Pia vipodozi hivyo hupunguza kwa sehemu kubwa tabaka la ngozi na kuifanya kuwa nyepesi ambapo hushindwa kuhimili miale ya mwanga inayopenya moja kwa moja mwilini. 

Licha ya kuwa jua lina umuhimu mkubwa mwilini lakini kama likikutana na ngozi isiyo imara linaweza kusababisha matatizo mbalimbali ikiwemo ngozi kujikunja, kuzeeka haraka, kansa na kupungua kwa kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa.  

Siyo ajabu kuwaona baadhi ya watu waliotumia mkorogo muda mrefu, ngozi zao zimejikunja na zina mabaka.  

Dk Elizabeth Lema kutoka kliniki ya tiba asili ya Cornwell Naturopathic iliyopo jijini Dar es Salaam anasema kwa ambao wanameza vidonge, wanabadilisha mfumo mzima wa vinasaba vya mwili na hali hiyo inaweza kuathiri hadi watoto watakaokuja kuzaliwa mbeleni.

“Anayemeza vidonge anabadilisha mfumo mzima wa seli ambapo ni kitu hatari sana kinachoweza kumsababishia mtu asizae kabisa au akizaa, watoto wasiwe kamili au akasababisha vinasaba vyake kuwa na shida na hivyo uzao wake kuwa na magonjwa fulani,” anasema mtaalam huyo wa afya.

Baadhi ya watu hununua bidhaa za kujichubua kwa bei rahisi bila kufahamu kuwa madhara yake ni makubwa kiafya na kiuchumi. Picha| WebMD.

Kwa wanaojipaka jiki wanaweza kupata matatizo ya figo na ini kwa sababu kemikali hizo huzuia utendaji wa viungo hivyo vinavyofanya kazi ya kundoa taka za mwili.  

Zaidi ya athari ndani ya mwili, mtu hulipa gharama kubwa za matibabu zinazoweza kumtumbukiza mtu katika umaskini wa kipato na kuzeeka mapema.

“Kibaya zaidi wanaotumia vitu hivi ni wale wenye kipato cha hali ya chini, hivyo hata wanapokuja kwa ajili ya matibabu, baadhi yao hushindwa kuyamudu kutokana na gharama yake,” anasema Dk Lema.

Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wanatumia vipodozi vya kujichubua na umeanza kupata madhara, zipo njia mbalimbali unazoweza kutumia kutoka katika mkwamo huo.  


Soma zaidi:


Ufanye nini kama umepata madhara ya kujichubua?

Huenda unajutia maamuzi uliyoyafanya miaka kadhaa iliyopita baada ya kupatwa na madhira mbalimbali ya kujichubua lakini safari yako bado ina matumaini.

Mshauri wa masuala ya kiafya kutoka kampuni inayotengeneza bidhaa za virutubisho ya Forever Living Products, Edmund Munyagi anasema kwa mtu ambaye ngozi yake imeharibika anatakiwa kula vyakula maalum vitakavyomsaidia kurejea katika hali ya kawaida. 

“Kuitunza ngozi yako unahitaji kula vyakula vilivyo na virutubisho na kunywa maji mengi ili kuipatia ngozi yako uhai,” anasema Munyagi.

Mshauri huyo wa bidhaa za afya amesema, kwa kuwa watu waliojichubua wameatiri ngozi yao kwa ndani na nje, wanahitaji kupata matibabu yatakayoondoa sumu ilijaa mwilini na kisha kutumia dawa au tiba lishe zitakazotumika kwenye ngozi ya nje.

Mmoja wa madaktari jijini dar es Salaam ameiambia Nukta kuwa endapo mtu amejichubua sana kiasi cha kuua melanin yote mwilini, huenda ikawa ni ngumu kwake kurejea hali yake ya awali.

“Kwa ambao wamejichubua kiasi cha kubakisha weusi sehemu za viwiko na vidole, kurudia hali yao ya kawaida inaweza kuwa ngumu au ikamgharimu fedha nyingi sana,” ameeleza mtalamu huyo aliyekataa kutajwa jina lake kulingana na sera za ofisi yake.

Usikose mwendelezo wa makala haya utakaoangazia jinsi ya kuitunza ngozi asilia kwa njia ambazo hazitokusababishia matatizo ya kiafya.