July 8, 2024

Hakuna kulala wahitimu kidato cha sita mwaka 2020

Wanatakiwa kujiunga na mafunzo ya JKT yatakayoanza Agosti 1 mwaka huu.

  • Wanatakiwa kujiunga na mafunzo ya JKT yatakayoanza Agosti 1 mwaka huu.
  • Wanatakiwa kuripoti katika makambi ya jeshi hilo walilopangiwa kati ya Julai 24 hadi 27, 2020.

Dar es Salaam. Kama wewe ni mhitimu wa kidato cha sita kwa mwaka 2020 na ulitarajia utarudi nyumbani na kupumzika ukisubiri matokeo ili kujiunga na elimu ya juu, fahamu bado una kibarua mbele yako. 

Kibarua hicho ni kujiunga na mafunzo maalum katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yatakayoanza Agosti 1 mwaka huu. 

Mitihani ya Taifa ya kidato cha sita iliyoanza Juni 29 imehitimishwa jana huku JKT nayo ikitangaza orodha ya majina 40,021 ya wahitimu waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya jeshi hilo ambayo yako kisheria. 

Taarifa ya JKT iliyotolewa Julai 17, 2020 imesema waliochaguliwa wanatakiwa kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza uzalendo, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha, utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa kupitia mafunzo hayo.

Vijana waliochaguliwa wamepangiwa katika kambi za JKT Rwamkoma mkoani Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu – Pwani, JKT Mpwapwa   Dodoma, JKT Mafinga – Iringa, JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba katika mkoa waTanga.

Kambi nyingine ni JKT Makuyuni – Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa, na JKT Mtabila – Kigoma, JKT Itaka – Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa – Rukwa, JKT Nachingwea – Lindi na JKT Kibiti- Pwani na Oljoro JKT- Arusha.

“Orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa, maeneo ya makambi ya JKT waliyopangiwa na vifaa wanavyotakiwa kwenda navyo inapatikana katika tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz”, amesema Kanali Kadawi.


Soma zaidi:  Kujiunga mafunzo ya JKT siyo ajira: Mwinyi


Amesema kuwa vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Julai 24 hadi 27, 2020 ambapo mafunzo yatafunguliwa rasmi Agosti 1, 2020.

Aidha, Kanali Kadawi amesema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa  macho  (Physical disabilities) wanatakiwa kuripoti katika kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa  jamii hiyo.

“Kutokana na Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu (COVID -19) nchini, tahadhari za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kama ilivyoelekezwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya zitazingatiwa kwa kipindi chote vijana watakapokuwa katika mafunzo,”, amesema Kanali Kadawi