October 6, 2024

Hakuna ugonjwa wa Ebola Tanzania-Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mpaka sasa hivi hakuna mgonjwa yeyote ambaye amethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania.

  • Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mpaka sasa hivi hakuna mgonjwa yeyote ambaye amethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania. 
  • Amewataka Watanzania kuchukua tahadhari ya kujikinda na kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini. 
  • WHO yatuma wataalam kuja nchini kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo. 

Dar es Salaam. Serikali imesema hakuna ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania na  kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini kutoka nchi  za jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC)

Hatua hiyo inakuja baada ya taarifa kuzagaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa ugonjwa huo umeingia nchini na baadhi ya watu wameanza kufariki kwa Ebola.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu aliyekuwa akitoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu ugonjwa huo leo (Septemba 14, 2019) jijini Dar es Salaam amesema mpaka sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola. 

“Wizara inawasihi wananchi, kutokuwa na hofu kwani mpaka sasa hivi hakuna mgonjwa yeyote ambaye amethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini Tanzania,” amesema Mwalimu.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na kudhibiti  ugonjwa huo ambao umeripotiwa katika nchi jirani usiingie nchini. 

“Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa Ebola umethibitika kuwepo nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambapo ilitolewa taarifa kwa mara ya kwanza Agosti 2018 na hadi kufikia Septemba 12, 2019,  kuna jumla ya wagonjwa 3,099 ambao wamethibitishwa kuwa na ugonjwa huo,” amesisitiza Mwalimu.


Soma zaidi:


Amesema  wizara yake  inapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa tangu ugonjwa huo uliporipotiwa katika nchi jirani imeweka mikakati na kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa ili usiingie nchini kwa kufanya masuala mbalimbali ikiwemo kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo kupitia katika wataalam wa afya katika mikoa, wilaya na maeneo ya mipakani.

Pia wizara imeimarisha uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipakani na kununua vifaa mbalimbali ikiwemo kipima joto, ambavyo wasafiri kutoka nchi mbalimbali wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo wamekuwa wakipimwa kabla ya kuingia nchini.

Aidha, Serikali imenunua na kusambaza seti takriban 2,700 za mavazi kinga kwenye mikoa yote iliyo katika hatari ya kukumbwa na tishio la Ebola ambayo mikoa hii ni Kigoma, Kagera, Mwanza, Rukwa na Katavi, kwa sababu inapakana na DRC.

Dalili kuu za ugonjwa wa Ebola ni homa kali, kuumwa na kichwa, kutapika, kuharisha, viungo vya mwili kuuma, kutokwa na vipele mwilini na kutokwa na damu katika matundu ya mwili.

Hata hivyo, amewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na kudhibiti  ugonjwa huo ambao umeripotiwa katika nchi jirani usiingie nchini. Picha|Mtandao.

WHO yaingilia kati uvumi wa Ebola Tanzania

Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia ukurasa wake wa tovuti kanda ya Afrika mjini Brazzaville, Congo, limesema kwa kushirikiana na mamlaka ya afya nchini Tanzania wanapeleka timu ya wataalam nchini humo kuchunguza fununu za kifo cha mtu mmoja kutokana na ugonjwa ambao haujajulikana bado.

WHO imewasiliana na wizara ya afya nchini Tanzania kupata taarifa zaidi na ikaelezea utayari wa kusaidia.

“Sambamba na wajibu wetu chini ya kanuni za kimataifa za afya, WHO mara kwa mara inapokea na kuchunguza uvumi wa masuala ya afya ya umma. Kwa msingi huo, WHO kwa kushirikiana na mamlaka inatuma wataalam nchini Tanzania kuchunguzi uvumi huo kama jambo la haraka.” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

WHO imesema itawasilisha matokeo ya uchunguzi wake kwa nchi wanachama baada ya kukamilika.