Halmashauri 10 bora matokeo kidato cha nne 2019
Bagamoyo imeungana na halmashauri zingine tisa ambazo zinaunda orodha hiyo ya dhahabu ya 10 zilizofanya vizuri kitaifa.
- Halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani imeshika nafasi ya kwanza kwa ufaulu kitaifa.
- Necta yazitaja Halmashauri zilizoshika mkia miaka mitatu mfululizo ikiwemo ya Malinyi ya mkoani Morogoro.
Dar es Salaam. Halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani imeshika nafasi ya kwanza kwa ufaulu kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne 2019 huku ikifanikiwa kuingiza shule moja katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.
Bagamoyo imeungana na halmashauri zingine tisa ambazo zinaunda orodha hiyo ya dhahabu ya 10 zilizofanya vizuri kitaifa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Masonde aliyekuwa akitangaza matokeo ya kidato cha nne leo kwa mpangilio wa ufaulu katika Halmashauri nchini amezitaja halmashauri zingine zilizofanya vizuri ikiwemo Bukoba Mjini na Meru mkoani Arusha.
Halmashauri ya Mafinga ambayo ilikuwa na shule 16 zilizoshiriki mtihani huo imeshika nafasi ya nne ikifuatiwa na Kibaha Mjini, Njombe Mjini, Kibondo, Kahama Mjini, Moshi na ya 10 ni Bariadi Mjini.
Kwa mpangilio wa matokeo hayo, mkoa wa Pwani umefanikiwa kuingiza Halmashauri mbili katika orodha hiyo.
Zinazohusiana
- Necta yatangaza matokeo kidato cha pili, nne 2019
- Matokeo kidato cha nne haya hapa
- Shule 10 bora zilizotikisa matokeo kidato cha nne 2019
Wakati watendaji wa halmashauri wakishangilia ushindi waliopata katika matokeo hayo, wenzao wa Halmashauri ya Malinyi mkoani Morogogo watakuwa katika tafakari baada ya halmashauri yao kushika mkia kitaifa.
Malinyi imeungana na halmashauri zingine tisa katika orodha ya halmashauri zilizofanya vibaya za Bumbuli ya mkoani Tanga, Kiteto (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpanda (Katavi). Zingine ni Kondoa ya mkoani Dodoma, Kakonko (Kigoma), Geita (Geita), Mafia (Pwani) na Kibiti (Pwani).
Halmashauri hizo zilizofanya ufaulu wake umeshuka kwa mika mitatu mfululizo na kuzifanya zing’ang’anie mkiani.
Katika orodha hiyo, mkoa wa Pwani umetoa halmashauri mbili huku mikoa iliyobaki imetoa shule moja moja.