October 6, 2024

Halmashauri zilizoshika mkia matokeo darasa la saba 2019

Wakati joto la kutangazwa kwa matokeo ya kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2019 likiwa bado halijapoa, orodha ya halmashauri 10 zilizofanya vibaya imetoka huku Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ikiwa ya mwisho kitaifa baada ya takriban nusu ya

  • Halmashauri ya Morogoro Vijijini imeshika mkia kitaifa kati ya halmashauri 186 zilizoshiriki mtihani huo Tanzania bara.
  • Takriban nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani huo katika halmashauri ya Morogoro Vijijini wamefeli.  
  • Halmashauri tano za Musoma Vijijini, Butiama, Mkalama, Chemba na Lushoto zimeingia kwa mara ya pili katika orodha hiyo.

Dar es Salaam. Wakati joto la kutangazwa kwa matokeo ya kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2019 likiwa bado halijapoa, orodha ya halmashauri 10 zilizofanya vibaya imetoka huku Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini ikiwa ya mwisho kitaifa baada ya takriban nusu ya wanafunzi waliofanya mtihani huo kufeli. 

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde aliyetangaza matokeo hayo Oktoba 15 alisema ufaulu umeongezeka kwa asilimia 3.8 ikilinganishwa na mwaka jana huku asilimia 81.5 ya watahiniwa 933,369 waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Katika taarifa ya mpangilio wa halmashauri kwa ubora wa ufaulu katika matokeo hayo iliyotolewa leo, imeonyesha kuwa Morogoro Vijijini imeshika mkia kitaifa kati ya halmashauri 186 zilizoshiriki mtihani huo Tanzania bara. 

Halmashauri hiyo, iliyokuwa na shule 156 zilizofanya mtihani huo mwezi Septemba, imeporomoka kutoka nafasi ya 128 iliyoshika mwaka jana kwa wanafunzi wake kufaulu kwa asilimia 53.8.

Hii ni ina maana kuwa takriban nusu ya wanafunzi wa halmashauri hiyo wamefeli kuendelea na masomo ya sekondari, jambo litakalowakosesha fursa mbalimbali zitokanazo na elimu ya sekondari na ya juu. 


Zinazohusiana:


Morogoro Vijijini ambayo iliyokuwa na watahiniwa waliosajaliwa 7,442  imeungana na halmashauri zingine tisa kuunda orodha hiyo ya halmashauri zilizofanya vibaya za Lushoto ya mkoani Tanga, Rorya (Mara), Chemba (Dodoma), Mkalama (Singida) na Butiama (Mara).

Nyingine ni Kondoa iliyopo Dodoma, Musoma Vijini (Mara), Liwale (Mtwara) na Hanang’ (Manyara). 

Hata hivyo, Halmashauri tano za Musoma Vijijini, Butiama, Mkalama, Chemba na Lushoto zimeingia kwa mara ya pili katika orodha hiyo, mwaka jana na mwaka huu.

Wakati halmashauri hizo zikitafakari jinsi ya kujikwamua katika mkwamo huo, Halmashauri ya Jiji la Arusha  ni kicheko tu kwa sababu imeshika nafasi ya kwanza kitaifa kwa ufaulu wa asilimia 97.6 ikiwa juu ya wastani wa kitaifa wa asimilia 81.5. 

Jiji la Arusha  imeungana na halmashauri zingine tisa zilizoingia 10 bora kitaifa za Ilemela, Kinondoni na Mwanza Jiji, Ilala Manispaa, Moshi Manispaa, Bukoba Manispaa, Iringa Manispaa, Biharamulo na Arusha.