Hatari iliyojificha nyuma ya vyakula vya kukaanga haraka
Vyakula vya aina hii zikiwemo chips na nyama za kukaanga vinavutia sana kuvila lakini vina madhara yake.
- Vyakula vya aina hii zikiwemo chips na nyama za kukaanga vinavutia sana kuvila lakini vina madhara yake.
Hakuna mazingira ya miji mikubwa ambayo utakatiza mitaa miwili pasipo kukutana na vibanda au migahawa walau mmoja wa chakula cha haraka hasa vile vya kukaanga maarufu kwa Kiingereza kama ‘Fast food’.
Mara nyingi sana vyakula hivi maarufu vikiwemo chips na kuku ama nyama za kukaanga hupendwa sana kwa sababu ya urahisi wake na uharaka wa kuandaa na upatikanaji hasa pale wahitaji wanapokua wengi.
Kimsingi huduma hii huhusisha utumiaji wa mafuta ya kula na kukaanga zaidi yaani “deep frying”, na mafuta haya huwekwa katika moto tangu mapishi yanapoanza hadi pale jiko linapozimwa.
Kwa maana nyingine ni kwamba kiwango cha mafuta hubadilishwa tu kwa kuongezea mafuta mabichi ikiwa yale yatapungua na mzunguko utaendelea hivyo hadi mwisho.
Katika mzunguko huu wa utumiaji wa mafuta, kuna mabadiliko ambayo hutokea hutokana na uzalishwaji wa joto linalosababisha kuachiliwa kwa kemikali tofauti tofauti zinazoweza kuleta athari katika mwili wa binadamu.
Kemikali hizi ni pamoja na oxidants na hydrogen peroxide. Sanjari na hayo, joto hili kali pia huathiri ubora mzima kabisa wa chakula.
Mafuta haya ambayo mengi huwa na kiwango kikubwa cha lehemu huongeza kiwango cha mafuta katika mwili na kukuweka katika hatari nzima ya magonjwa ya moyo na mishipa.
Maana yake ni kwamba unajiweka katika uwezekanao wa mafuta kurundikana na kuziba njia ya damu na kufanya damu ishindwe kupita kwa ufanisi katikati.
Mara nyingi sana vyakula hivi maarufu vikiwemo chips na kuku ama nyama za kukaanga hupendwa sana kwa sababu ya urahisi wake na uharaka wa kuandaa na upatikanaji hasa pale wahitaji wanapokua wengi. Picha|Andy Wangy/Unsplash.
Ugumu huu husababisha damu kusukumwa kwa nguvu zaidi na kusababisha shinikizo la juu la damu.
Hilo halitoshi, wakati mwingine vijibonge hivi vya mafuta huweza kumeguka na kujiingiza katika mzunguko wa damu wa kawaida. Hapa ndipo kiharusi huanza kunyemelea kwa kuwa vijibonge hivi huweza kuingia katika mishipa midogo iendayo katika ubongo na kusababisha ukosefu wa damu eneo hilo.
Ukosefu wa damu humaanisha kukosa oksijeni na sukari mfumo wa glucose ambao ni muhimu kwa utendaji wa seli na tishu za ubongo. Hapa mtu hujiweka katika mazingira ya kupata kiharusi.
Uchemkaji usioisha wa mafuta haya pia husababisha uzalishwaji wa kemikali ya ‘hydrogen peroxide’ ambayo kimsingi tumezungukwa nayo kwa kuwa hutumika majumbani katika bidhaa za kusafishia vyoo, kufulia na hata bidhaa za usafi wa kinywa.
Lakini zote hizi huwa katika kiwango kidogo ambacho hutosheleza tu kwa matumizi hayo bila kuwa na athari kubwa katika mwili. Utafiti unaonesha kuwa watu wengi hujiweka katika mazingira ya kumeza hydrogen peroxide mara kwa mara kwa ulaji wa bidhaa hizi uliokithiri.
Kadhia zinazoweza kuambatana na hydrogen peroxide ni kuathiri mfumo mzima wa upumuaji na hewa na mtu huweza kupata miwasho.
Kadhia nyingine ni kutapika, mfumo wa chakula kuathirika na wakati mwingine japo sio mara kwa mara kuziba kwa mishipa ya mfumo wa chakula kutokana na kemikali hii.
Namna ya kupunguza madhara
Ni vyema sana kwa wahusika kuwa na kiasi katika matumizi ya vyakula vya haraka. Lakini pia wapishi na waandaaji katika migahawa mikubwa na midogo kuwa na utaratibu wa kubadili mafuta na kuepuka kutumia mafuta hayo hayo kwa muda mrefu.
Hata hivyo, jukumu la kutunza afya muungwana mwenzangu ni suala la demokrasia yaani lina mhusu mtu mmoja mmoja na la kujiamulia.
Ushauri na hoja yangu ni kwamba, jitahidi sana kupunguza matumizi au ulaji wa vyakula vya migahawa ambavyo hutokana na kukaanga. Usiwe utaratibu wako wa kila siku ili kujiweka katika mstari sahihi wa usalama wa afya yako.