July 1, 2024

Hatma fedha za wateja wa benki ya FBME bado bado sana

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema hatma ya fedha za wateja wa benki ya FBME iliyofungwa itajulikana mara baada ya zoezi la ufilisi na uuzaji wa mali za benki hiyo kukamilika.

  • Ni benki iliyonyang’anywa leseni na BoT mwaka 2017.
  • Serikali yasema wateja wake watalipwa mpaka zoezi la ufilisi likamilike.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema hatma ya fedha za wateja wa benki ya FBME iliyofungwa itajulikana mara baada ya zoezi la ufilisi na uuzaji wa mali za benki hiyo kukamilika. 

May 8, 2017 FBME ilinyang’anywa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo ni mlezi wa benki nchini kutokana na kushindwa kujiendesha na kukabiliwa na changamoto za mtaji. 

Dk Nchemba aliyekuwa akizungumza leo (Aprili 21, 2021) bungeni jijini Dodoma amesema huenda zoezi la uhakiki na uuzaji wa mali za benki hiyo likachukua muda mrefu na hivyo wateja wa benki hiyo wawe na subira. 

“Sasa zoezi hilo kukamilika linachukua muda kuhakiki mali lakini pia uzibadilishe ziwe fedha linachukua muda, hicho ndicho kinachelewesha. Sasa ni lini itakamilika, nakumbuka utaratibu ulikuwa unaendelea na umefikia hatua nzuri,” amesema Waziri huyo.

Nchemba alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Catherine Magige aliyetaka kufahamu kauli ya Serikali kuhusu hatma ya fedha za wateja wa benki hiyo iliyofungwa.

“Iliyokuwa benki ya FBME sasa ni zaidi ya miaka 4 tangu BoT waifunge, wananchi wa Arusha na sehemu mbalimbali waliokuwa na akaunti katika benki hiyo hadi leo hawajui hatma ya pesa zao,” amesema Magige katika swali lake.


Zinazohusiana: 


Katika ufanunuzi wa Dk Nchemba amesema kilichochelewesha mgawanyo wa fedha ni utaratibu wa kawaida ambao mfilisi anatakiwa kukamilisha hatua zote za ufilisi wa benki husika.

“Zoezi la mfilisi likamilike kwanza na zoezi hilo linahusu mali zote zilizopo zikusanywe, ziuzwe halafu zigeuzwe kuwa fedha,” amesema Nchemba ambaye ni Mbunge wa Ilamba Mashariki.

Uamuzi wa BoT kuifungia benki hiyo ulitokana na notisi iliyotolewa July 15 2014 na Taasisi ya Marekani inayopambana na uhalifu wa kifedha (The US Financial Crimes Enforcement Network”(FinCEN)), iliyoituhumu FBME kuwa ni taasisi inayojihusisha na biashara ya utakatishaji wa fedha haramu na hatua ya Benki Kuu ya Cyprus kuliweka tawi la FBME lililopo nchini Cyprus chini ya uangalizi maalumu (special administration).

Kutokana na tatizo hilo benki hiyo ilishindwa kufanya miamala ya kibenki ya kimataifa na kupata huduma za mifumo ya kibenki na hivyo kushindwa kutoa huduma muhimu kwa wateja wake kwa mujibu wa leseni waliyopewa.