October 8, 2024

Haya ndiyo maisha anayotakiwa kuishi bachela

Anatakiwa kuwa mkweli, kuishi kulingana na kipato chake na kujiandaa vema kutimiza malengo binafsi na familia yake hapo baadaye.

  • Penda kuwa mkweli na honga kwa kiasi.
  • Epuka kuishi mbali zaidi na kazini kwako ili kupunguza gharama za usafiri.
  • Punguza gharama zisizo za lazima.

Dar es Salaam. Pale tu unapoanza safari ya ujana wako, unategemewa kukutana na vihunzi na milima mirefu kufikia mafanikio hasa kama wewe siyo “wakishua”.

Safari yako inaweza kuwa ngumu zaidi pale ambapo unataka kutumia zaidi ya kipato chako ili tu kuwaonyesha watu wakuone na wewe uko mjini. Lakini huenda unavyofanya hivyo bila kuwa na maarifa kuwa unajiwekea changamoto kubwa ya kufikia mafanikio uliyokusudia. 

Kwanini uhangaike na kuweka ujana wako kwenye nafasi ambayo hata mara zingine “shetani” anakushangaa pale unapomsingizia? Zingatia haya ili uishi kulingana na kipato ulicho nacho.

Kuwa na mpenzi mmoja

Ni kawaida kwa baadhi ya mabachela huwa na mpenzi  lakini baadhi yao huwa na zaidi ya mmoja na hivyo kuhudumia mara mbili.

Unahisi hauhudumii? Ni mara ngapi umetuma vocha au kumtoa mpenzi wako kula chipsi na kuku wa KFC? Basi ushaelewa ni nini ninazungumzia.

Kwa kuwa na mpenzi mmoja itakusaidia kubaki kwenye bajeti yako na zaidi kujipunguzia matumizi ya ziada yasiyo na mpangilio. Pia, kama unaye mpenzi mmoja wa kweli, ni rahisi hata kumueleza hali yako ya kiuchumi na akakuelewa.

Ni mara ngapi umetuma vocha au kumtoa mpenzi wako kula chipsi na kuku wa KFC? Basi ushaelewa ni nini ninazungumzia. Picha| Bonobology.

Panga eneo unalolimudu

Hii ni kwa wale waliopanga kwenye vyumba mbali na kwao. Endapo unafanya kazi au harakati zako mjini, ni hekima kufanya shughuli hizo karibu na eneo lako la kazi ili kukupunguzia gharama za usafiri.

Hauna haja ya kuishi Kimara huku kazi zako zipo Posta kwani mbali na usafiri kuwa wa shida, zipo siku utakazojikuta unatumia zaidi ya bajeti yako kwenye usafiri badala yake, tafuta makazi Kinondoni ambapo utapata gari moja na utatumia muda mfupi.

Pia, unaweza kufikiri kuishi Tabata ambapo magari ya kivukoni ni Sh500 tu

Ninazungumzia zile siku ambazo mwendokasi “umebuma” na bosi wako hawezi kukuelewa hivyo itakulazimu uchukue pikipiki au chombo kingine kuwahi kazini.


Honga kwa kiasi

Unawezaje kuhonga simu wakati wewe simu yako ulinunuliwa na baba yako kipindi cha kuanza chuo?

Hii ni kwa “Ma gentlemen” zaidi. Endapo una mpenzi wako, jitahidi kumpenda kwa uwezo wako, kama uwezo wako ni wa kununua peremende na viatu, hauna haja ya wewe kutaka kumfanyia makubwa yatakayoishia kukukondesha kwa mawazo.

Ni kweli kama njemba unatakiwa “kumspoil” mpenzi wako kwa “vijisuprise” na mitoko mara kadhaa lakini kama mpenzi wako anafahamu hali yako, yanini uhangaikie kumnunulia pizza wakati mihogo ya mama Juma ipo, cha muhimu ni muda wako, ukweli wako na udhati wa mapenzi yako.


Zinazohusiana


Panga bajeti

Japo ni jambo gumu kwa wengi, bajeti ni kitu muhimu kwa kila mtu anayehitaji kujikwamua kiuchumi.

Kupitia bajeti, utapata nafasi ya kuweka akiba ambayo itakusaidia kufikia ndoto zako na zaidi, itakufanya utumie fedha kwa nidhamu.

Jifunze kula kwa bajeti yako, “kuspend” kwa bajeti yako na kuwekeza kwa bajeti yako. Itakusaidia kuwa na amani na kuepukana na mawazo ya “kesho nitakula nini”.

Jifunze kula kwa bajeti yako, “kuspend” kwa bajeti yako na kuwekeza kwa bajeti yako. Picha| Campaign Creators/Unsplash.

Kuwa mkweli

Huenda zile simu za “nisaidie 50,000” zinatokana na uongo ambao unawaambia masela zako.

Kwenye zile stori za uongo na kweli unazodanganya wakati wa kupiga madili ya milioni mbili, yupo msela wako anayekuona kama msaada kwake pale anapokuwa na shida.

Zaidi, pale unapomdanganya mpenzi wako kuwa unafanya kazi benki hali inazidi kuwa mbaya pale anapokutafuta mwisho wa mwezi na kukuomba umsaidie pesa kwa ajili ya dharula fulani.

Unaweza kuyakwepa hayo yote kwa kuwa mkweli na kuishi maisha ya hadhi yako kwa wakati huo kwani wala hakuna anayeshindana na wewe.

Usijitese, kila hatua ya maisha ina mambo yake. Ya nini ung’ang’ane kuvaa suti wakati nepi bado? Usikose kusoma “yanayokuhusu” ijumaa ijayo.