October 6, 2024

Haya ndiyo makubaliano ya Rais Samia na Kenyatta

Rais Samia Suluhu Hassan amesema amefanya mazungumzo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambapo wamekubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kukuza na kuimarisha uhusiano na mshikamano kati ya mataifa hayo mawili.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na mwenyeji wake Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi leo. Picha: Ikulu ya Kenya.


  • Kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi kati ya nchi hizo ili kurahisisha biashara.
  • Kuimarisha ushirikiano na kuondoa mizozo isiyokuwa ya msingi.
  • Rais Kenyatta pia ameshauri kufufuliwa safari za mizigo na abiria kupitia Ziwa Victoria.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema amefanya mazungumzo na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambapo wamekubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kukuza na kuimarisha uhusiano na mshikamano kati ya mataifa hayo mawili.

Akihutubia waandishi wa habari nchini Kenya leo (Mei 4, 2021) baada ya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia amesema umefika wakati wa Tanzania na Kenya kuangazia misingi ya kiuwekezaji katika nyanja mbalimbali zikiwemo utalii, kilimo, ufugaji na viwanda.

Amesema yeye na Rais Kenyatta wamekubaliana kuondoa vikwazo vizivyo vya kikodi ili kuimarisha biashara kati ya nchi hizo.

“Tumekubaliana kuendelea kushughulikia baadhi ya changamoto hususan vikwazo visivyo vya kodi vinavyotokea katika mipaka yetu sasa vindoke na tumeitaka tume yetu ya ushirikiano baina ya Kenya na Tanzania iwe inakaa na kutoa suluhu ya vikwazo vinavyojitokeza,” amesema Rais Samia. 

Pia wamekubaliana mawaziri wa Afya wa nchi hizo waongee kuona namna ya kurahisisha muingiliano wa kibiashara kati ya Kenya na Tanzania katika kipindi hiki cha Corona.

“Mbali na uwekezaji nchi za Tanzania na Kenya ni wadau wakubwa wa biashara ambapo kwenye miaka mitano iliyopita wastani wa biashara kati ya nchi hizi ni Dola za Kimarekani milioni 450 (Sh1.1 trilioni) ambayo bado siyo kubwa na tumeweka ahadi kuikuza,” amesema.

Aidha, amemwalika Rais Kenyatta kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika yatakayofanyika Desemba mwaka huu huku akisema migogoro midogo midogo kati ya nchi hizo mbili haina budi kumalizika.

Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini Tanzania ikitanguliwa na mataifa mengine kutoka nje lakini ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki Kenya ni ya kwanza. 

“Kenya imewekeza miradi 513 yenye thamani ya Dola za Kimarekani 1.7 bilioni (Sh 3.9 trilioni) ambayo imetoa ajira zipatazo 51,000 za Watanzania. Aidha zipo kampuni 30 za Tanzania ambazo zimewekeza mtaji ndani ya Kenya wenye thamani ya Ksh 19.33 bilioni (Sh410.8 bilioni) na kutoa ajira kwa watu 2,640,” amesema Rais Samia. 


Soma zaidi:


Hii ni mara pili kwa Rais Samia kufanya ziara ya kikazi nje ya nchi tangu alipoapishwa kuwa Rais wa sita wa Tanzania Machi 19 mwaka huu baada ya kifo cha Hayati Rais John Magufuli. 

Mwezi Aprili alitembelea Uganda ambapo alikutana na Rais Yoweri Museveni katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki lenye urefu wa kilometa 1,443 kutoka Hoima nchini humo hadi katika bandari Tanga. 

Kwa upande wake Rais Kenyatta amesema yeye na Rais Samia wamekubaliana kuanza ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa ambalo litahakikishia viwanda vya kenya nishati safi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda nchini humo.

“Tukiweza tena kuanzisha safari zetu zile zilikuwa zipo kule Ziwa Victoria wakati wananchi na mizigo ilikua inatembea kutoka upande ya Jinja kuja Kisumu kuelekea kule Mwanza na Bukoba na ikarahisisha wakati huo mwenendo wa wananchi wetu na kuzalisha biashara kati ya wananchi wetu,” amesema Kenyatta.