November 24, 2024

Haya yanaweza kuisadia chaneli mpya ya Utalii Tanzania kuifikia dunia kirahisi

Wadau wanashauri zifanyike tafiti nyingi zitakazoisadia chaneli hiyo kuwafikia watalii wengi duniani na kuajiri wazalishaji bora wa maudhui ya safari.

Mategemeo ya watazamaji wa chaneli ya Safari ni kuona zaidi ya wanyama kwenye chaneli hiyo.Picha| Tanzaniatoday

  • Wataalam wa maudhui na utaliii wanashauri kufanyika tafiti nyingi ili kuzalisha vipindi vitakavyowavutia watalii wengi kutoka pande mbalimbali za dunia.
  • Waonyesha wasiwasi wao juu ya mfumo utakaokuwa unatumia kutafsiri lugha kama utakuwa wa maandishi au ule wa kuingizia sauti.
  • Washauri kitengo cha masoko na promosheni kuwa wabunifu kwa kuleta kauli mbiu zitakazowavutia zaidi watalii na kwa lugha inayoeleweka.
  • Bosi wa TBC amesema wameanza mazungumzo na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo DStv kuhakikisha chaneli hiyo inawafakikia wengi zaidi duniani.

Dar es Salaam. Baada ya Serikali kuzindua chaneli mpya ya Safari inayolenga kutangaza utalii wa Tanzania, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na wadau wanaoshirikiana nao watakuwa na vibarua vikuu viwili; kutengeneza maudhui bora yenye kuvutia na kuhakikisha yanawafikia watu wengi zaidi maeneo mbalimbali ulimwenguni ili kufikia malengo yanayotarajiwa.

Hivi karibuni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizindua chaneli hiyo jijini Dar es Salaam huku akieleza kuwa italisaidia Taifa kupata idadi kubwa ya watalii, kuongeza fedha za kigeni na kuongeza Pato la Taifa (GDP).

Majaliwa, anayetamani chaneli hiyo iwe huru na kupewa jina la TBC3, alisema itafungua milango ya ajira kwa watu mbalimbali wakiwemo wananchi ambao watanufaika na shughuli na biashara ya utalii katika maeneo yenye vivutio nchini.

Matamanio yake na msisitizo ni kwamba wafanyakazi wa chaneli hiyo wapatiwe fursa ya kwenda kujifunza zaidi ili kuiendesha chaneli hiyo kisasa ifikie viwango vya chaneli ya Discovery ya nchini Marekani.

Ili kuwa na viwango vya juu vya maudhui na kufikia watalii wengi zaidi ulimwenguni kama Serikali inavyotaka, baadhi ya wataalam wa maudhui na utalii wameiambia nukta.co.tz kuwa TBC na wabia wengine wa chaneli hiyo wanapaswa kuwekeza zaidi katika rasilimali watu, tafiti za mara kwa mara kuboresha maudhui na masoko.

“Chaneli hii inahusisha wadau wengi kwa kuinadi ni ya TBC pekee inaweza kufanya wengine wasipende kuangalia hivyo promosheni zionyeshe wameshirikiana na wengine,” anasema Dk Vicensia Shule, Mtaalamu wa uzalishaji maudhui.

 

Utamaduni wa kimasai ni moja ya kivutio cha watalii kuja kutembelea vitu mbalimbali nchini. Picha|www.pulselive.co.ke

Dk Shule ameiambia Nukta kuwa bado chaneli hiyo inahitaji kuendeshwa zaidi na tafiti kuangalia watalii wanataka nini kuliko kuangalia wazawa wanataka nini kwa sababu pesa nyingi za utalii ni zao la watalii wa nje.

Tafiti za kwenda kujifunza namna masoko makubwa ya utalii kama nchi za China, Singapore, Korea Kusini, Brazil, Namibia, Afrika Kusini na nyinginezo yanavyofanya, kwa mujibu wa Dk Shule, zitasaidia chaneli hiyo kuwa endelevu na kufanikisha malengo ya chaneli hiyo.

“Lazima kuwepo kwa vipindi zaidi ya wanyama, yaani kuwe na historia za makabila mbalimbali, vyakula vya asili pamoja na vitu vitakavyofanya watalii wavutike kuja kila siku na bila kusahau kuwepo kwa vipindi mchanganyiko visivyo na marudio mara kwa mara,” amesema.

Tayari Majaliwa alishawaagiza waendeshaji wa chaneli hiyo kutumia marafiki na balozi mbalimbali ambazo wanaweza kupeleka wafanyakazi kujifunza ili waendeshe vipindi kwa ufasaha na kisasa zaidi.

Hata hivyo, uzinduzi wa  chaneli hiyo muhimu nchini unakuja katika kipindi ambacho chaneli mbalimbali za kitaifa zisizolipiwa (Free-to-Air) zikiwa zimeondolewa katika visimbuzi maarufu vya Zuku, DStv, AZAM. 


Zinazohusiana: 


Kuondolewa kwa chaneli hizo katika visimbuzi hivyo, vinavyotoa huduma hadi katika nchi jirani, kumeleta sintofahamu miongoni mwa watazamaji wengi huku wamiliki wake wakisema kutapunguza idadi ya watazamaji na kuwanyima haki yao ya kupata habari.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayub Rioba ameiambia Nukta kuwa wameanza mazungumzo na wadau wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha chaneli mpya ya utalii inawafikia watu wengi na kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini.

“Tunataka kuhakikisha inapatikana kila mahali, tupo kwenye mazungumzo na wadau kama DSTV na wengine ili tuweze kufika maeneo mengi duniani,” amesema Dk Rioba.

Uzinduzi wa chaneli unaongeza stesheni za luninga nchini ambazo hadi Desemba 2017, takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinabainisha kuwa kulikuwa na vituo 48 huku takriban kimoja kati ya vitatu kikiwa kinatoa huduma kwa njia ya ‘cable’.

Hivyo uzinduzi wa chaneli hiyo unaleta ushindani mpya katika soko la luninga nchini hasa kwa vituo ambavyo vilikuwa vikirusha maudhui ya aina hiyo hapo awali.

“Waweke hata vipindi kuhusu nyota za angani kwa kuwa baadhi ya nchi hawazioni na hali ya hewa kwa sababu sisi ni nchi ambayo tunapata jua masaa 12 kitu ambacho kuna wengine hakuna, hivyo tujaribu kujipambanua vizuri kwenye maudhui ya vipindi,” anasema Dk Melubo Kokel, Mhadhili wa Chuo cha Wanyama Pori cha Mweka.

Hata hivyo, kwa upande wa lugha itakayotumika bado wengi wanapata mashaka kama itafikisha ujumbe kwa watalii wanaokusudiwa ili kuweza kufikia malengo ya kukuza utalii kupitia chaneli hiyo.

Lakini Dk Rioba anaeleza kuwa watatumia lugha ya Kiswahili na kutafsiri kwa Kichina, Kihindi, Kiingereza, Kirusi na nyinginezo ambazo ni soko kubwa la watalii.

“Inabidi kama kutafsiri basi tutumie watu wanaojua kuongea lugha hizo ambao watakuwa wanasaidia kufikisha ujumbe sehemu husika, bado narudia tena tafiti ziendelee kufanyika,” anasema Dk Shule.

Hata hivyo, juhudi hii ya Serikali na wadau wa utalii imepongezwa  lakini  wanashauri ili ilete faida inabidi waliopo kwenye kitengo cha masoko na promosheni wanatakiwa kuwa wabunifu kwa kuleta kauli mbiu zitakazowavutia zaidi watalii na kwa lugha inayoeleweka.

“Chaneli ni ya burudani waache kuweka mambo ya uzalendo inaboa, mtalii haitaji hayo,” amesema Dk Shule.

Licha ya kuwepo kwa matumaini makubwa ya chaneli hiyo  Dk Kokel anawashauri watafutaji masoko kuwekeza zaidi kupata soko la China, Urusi, Marekani ya kusini na Uarabuni kwasababu ndipo watalii wengi walipo.