November 24, 2024

Haya yatasaidia kukuza ubunifu wa teknolojia Tanzania

Wadau washauri kujenga vituo vya ubunifu katika mikoa yote nchini ili kuwapa fursa vijana ambao hawajaelimika.

  • Washauri kujenga vituo vya ubunifu katika mikoa yote nchini ili kuwapa fursa vijana ambao hawajaelimika. 
  • Elimu na mafunzo yatawasaidia vijana kulinda na kuendeleza kazi zao ubunifu.
  • Jamii nayo itafaidika na fursa za ajira na kuondokana na umasikini.

Dar es Salaam. Wadau walioshiriki warsha ya siku moja ya kusikiliza kazi za kibunifu kwa kampuni zinazochipukia wameshauri Serikali na taasisi zinazohusika kuendeleza ubunifu kuongeza wigo kutoa mafunzo na kuwafikia vijana wa rika zote ili kujenga mfumo wa teknolojia utakaosaidia kutatua changamoto za jamii ikiwemo umasikini na ukosefu wa ajira. 

Wito huo umekuja wakati mafunzo yanayotolewa kuendeleza ubunifu wa teknolojia yamekuwa yakitolewa zaidi kwa wahitimu wa vyuo vikuu ambao wanapatikana maeneo ya mjini. 

Warsha hiyo iliyofanyika leo (Februari 19, 2019) jijini Dar es Salaam imewakutanisha wadau wa maendeleo na ujumbe wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) kusikiliza mawazo, kujionea kazi za baadhi ya kampuni zinazochipukia ikiwemo Nukta Africa na kuangalia namna ya kutengeneza ubia na uwekezaji utakaosaidia kampuni hizo kutatua changamoto katika jamii. Nukta Africa inamiliki tovuti hii ya habari ya nukta.co.tz. 

Aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dr Hassan Mshimda amesema vituo vya kuendeleza ubunifu na teknolojia vinapaswa kujitanua ili kuwafikia vijana wengi waliopo katika maeneo mbalimbali kwa kuwa mfumo wa Tehama unawawezesha kuanzisha kampuni.

Amesema sambamba na hilo ni kuwawezesha vijana wenye mawazo ya kibunifu kulinda na kuziendeleza haki miliki (Intellectual Property) ili kuwaongezea mapato na kupata mitaji ya uwekezaji. 

Costech kwa kushirikiana na vituo vya kijamii vya ubunifu na teknolojia kama Bun Hub, Kinu Hub na Seedspace wamekuwa mstari wa mbele kuinua vipaji na ubunifu wa vijana wanaotumia Tehama kuifikia jamii inayowazunguka.


Zinazohusiana: 


 Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Foundation for Civil Society amesema jitihada za kuendeleza Tehama nchini ziwafikie vijana wote hata wale ambao hawajaelimika ili kujenga msingi tangu ngazi ya chini wa mawazo ya kibunifu kuisaidia jamii.

Amesema ubunifu ukiwekewa mikakati mizuri unaweza kusaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Vituo vingi na mafunzo ya ubunifu yanapatikana maeneo ya mijini, jambo linalokwamisha baadhi ya maeneo kuondokana na umaskini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Nukta Africa, Nuzulack Dausen akitoa maelezo juu ya utendaji wa kampuni hiyo iliyowekeza katika teknolojia na habari za takwimu. Picha|Zahara Tunda.

Hata hivyo, wadau hao watakuwa na kazi kubwa ya kuwafikia vijana wengi waliopo vijijini ikizingatiwa kuwa takriban nusu ama asilimia 48 ya vituovya ubunifu nchini (Innovation hubs) vipo jijini Dar es Salaam huku vilivyosalia vikitawanyika katika mikoa mbalimbali. 

Kwa mujibu wa ripoti ya mtawanyiko wa vituo vya ubunifu Tanzania iliyolewa Desemba 2018 na Mfuko wa Kuendeleza Rasimali Watu (HDIF) inaeleza kuwa mpaka sasa kuna vituo vya ubunifu 43 ambapo karibu nusu ya vituo hivyo (asilimia 48) vinapatikana Dar es Salaam. 

Licha ya kuwepo kwa changamoto kama kukosekana kwa ushirikiano wa wadau wa teknolojia, Maneja Mkuu wa kampuni ya uwekezaji na ujasiriamali wa teknolojia ya Seedspace, Innocent Mallya amesema bado Tanzania ina nafasi ya kuendeleza Tehama ikiwemo kujenga vituo hivyo katika mikoa mengine nchini. 

Amesema vituo hivyo vitasaidia kuvutia mitaji ya uwekezaji kutoka kwa wawekezaji na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wenye mawazo ya kibunifu.