Hesabu zaendelea kuwatoa jasho wanafunzi kidato cha nne Tanzania
Kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2020, ni asilimia 20.1 tu ya watahiniwa 434,654 waliofanya mtihani huo, ndiyo wamefaulu somo la hisabati
- Ufaulu wake uko chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 50.5 mwaka 2020.
- Wanafunzi nane kati ya 10 wamefeli somo hilo.
- Wachambuzi wa elimu wasema ifanyike tathmni ya kitaifa kutafuta suluhu ya changamoto ya kufeli kwa wanafunzi katika somo hilo.
Dar es Salaam. Wataalam wa elimu Tanzania wamependekeza kufanyika kwa tathmini ya kitaifa ili kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo la watahiniwa wa kidato cha nne kufeli zaidi somo la hisabati kila mwaka.
Kwa mujibu wa matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2020 yaliyotangazwa Januari 15 mwaka huu na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), ni asilimia 20.1 tu ya watahiniwa 434,654 waliofanya mtihani huo, ndiyo wamefaulu somo la hisabati (Basic Mathematics).
Hiyo ni sawa na kusema kwa kila watahiniwa 10 ni wawili tu ndiyo wamefaulu somo hilo ambalo linatajwa kama “ugonjwa wa Taifa kwa elimu ya Tanzania”.
Kiwango hicho cha ufaulu wa hisabati ndiyo cha chini kabisa ikilinganishwa na masomo mengine huku wanafunzi wakiwa wamefanya vizuri zaidi katika somo la Kiswahili ambapo asilimia 94.8 ya watahiniwa wamefaulu.
Ufaulu wa Kiswahili ni zaidi ya mara nne ya ule wa somo la hisabati, somo ambalo ni lugha ya Taifa na ambalo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu nchini, wamekuwa wakipendekeza itumike kama lugha ya kufundishia darasani ili kuwaongezea wanafunzi uelewa wa masomo.
Somo lingine ambalo wanafunzi hawajafanya vizuri ni fizikia (Physics) ambapo ufaulu wake ni asilimia 48.8. Somo hilo linaungana na hisabati ambapo yote mawili, ufaulu wake uko chini ya wastani wa kitaifa ambao ni asilimia 50.5.
“Takwimu za matokeo zinaonyesha kuwa watahiniwa hawakufanya vizuri katika masomo mawili ya Fizikia na Basic Mathematics, japokuwa katika somo la Physics ufaulu umeendelea kuimarika kutoka asilimia 48.38 kwa mwaka 2019 hadi asilimia 48.87 kwa mwaka 2020,” alisema Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde wakati akitangaza matokeo hayo.
Ufaulu wa miaka ya nyuma ukoje?
Licha ya kuwa hisabati ni muhimu kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi, bado limekuwa likiwatesa zaidi wanafunzi katika ngazi zote za elimu ikiwemo kidato cha sita.
Ufaulu wa mwaka 2020 hauna tofauti sana na miaka iliyotangulia. Mathalan, katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2019, ni asilimia 20.1 ya wanafunzi ndiyo waliofaulu somo hilo.
Ufaulu wa 2020 unaofanana kabisa na wa mwaka 2019 umeongezeka kidogo kutoka asilimia 19.2 wa mwaka 2018. Hali hiyo pia imekuwa ikijitokeza kwa miaka iliyotangulia.
Wachambuzi wa elimu watoa mwelekeo mpya
Wakati wazazi na wanafunzi wakibaki na maswali juu ya ufaulu usioridhisha wa hisabati, wachambuzi wa masuala ya elimu wamependekeza ifanyike tathmini ya kitaifa ili kukusanya maoni yatakayobainisha kiini cha tatizo la wanafunzi kufeli somo hilo kila mwaka.
Mwalimu na mwandishi wa vitabu mashuhuri, Richard Mabala amesema Serikali na wadau wa elimu wanapaswa kufanya utafiti ili kuwauliza walimu na wanafunzi kuhusu mambo yanayokosekana ambayo yanafanya ufaulu wa somo hilo uwe chini.
“Wafanye utafiti, waulizwe walimu na wanafunzi kwanini wanafeli, wao ndiyo wana majibu ya changamoto hiyo,” amesema Mabala ambaye pia ni Mwenyekiti wa bodi ya Shirika la HakiElimu Tanzania ambalo linahusika na masuala ya elimu Tanzania.
Majibu hayo, kwa mujibu wa Mabala, yatasaidia katika utengenezaji wa mitaala rahisi itakayowasaidia wanafunzi kuongeza ufaulu wa somo hilo.
Soma zaidi:
Suluhu nyingine itakayosaidia kuongeza ufaulu katika somo hilo, ni kubadili mtazamo miongoni mwa wanafunzi na walimu kuwa somo hilo ni gumu na lichukuliwe kama masomo mengine. Mbali na kufanya utafiti kugundua kiini cha tatizo, baadhi ya wataalamu wa elimu wanashauri wanafunzi kuanza kufundishwa saikolojia ya masomo ya sayansi na hisabati itakayofanya wayaone na uzito unaofanana.
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DUCE), Dk Luka Mkonongwa ameieleza Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa saikolojia ya masomo hayo itawasaidia wanafunzi kuona kuwa hakuna somo kama inavyodhaniwa.
“Walimu wanatakiwa wawafundishe wanafunzi kwa upendo, uvumilivu na kuwatia moyo kuwa hesabu siyo ngumu huku wakitafuta njia rahisi za ufundishaji wa somo hilo,” amesema Dk Mkonongwa.
Mchambuzi huyo wa masuala ya elimu amesema pia walimu wanaofundisha somo hilo wanapaswa kunolewa vizuri ili kuhakikisha wana uelewa mzuri wa utaokasaidia kueleweka wanapofundisha wanafunzi darasani.
Dk Mkonongwa amesema ifike mahali ufundishaji wa hisabati uhusianishwe na mazingira halisi ya maisha na siyo nadharia ambazo haziwasaidia wanafunzia baada ya kujifunza.
“Wanafunzi watapenda somo hilo kama wataambiwa linawasaidia nini kwenye maisha yao. Waambiwe wanawezaje kutumia hesabu kwenye shughuli zao ikiwemo ufundi,” amesema mtaalam huyo wa elimu huku akibainisha kuwa mitaala ya somo hilo iangaliwe upya ili iendane na hali halisi ya wakati huu.
Mhadhiri huyo anaungana na Mabala kuwa kuna haja ya kufanyika tathmini ya kitaifa ili ipatikane suluhu ya kudumu ya ufaulu wa somo hilo.