HESLB yafungua dirisha waliokosa mikopo kukata rufaa
Rufaa hiyo ni kwa wanafunzi ambao hadi sasa hawajapata mkopo au hawajaridhika na kiwango cha mkopo walichopangiwa katika mwaka wa masomo wa 2019/2020.
- Dirisha la kuwasilisha rufaa hizo liko wazi kuanzia Novemba 13 had 23, 2019.
- Rufaa hiyo ni kwa wanafunzi ambao hadi sasa hawajapata mkopo au hawajaridhika na kiwango cha mkopo walichopangiwa katika mwaka wa masomo wa 2019/2020.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua dirisha la kukata rufaa kwa wanafunzi ambao hadi sasa hawajapata mkopo au hawajaridhika na kiwango cha mkopo walichopangiwa katika mwaka wa masomo wa 2019/2020.
Taarifa ya HESLB iliyotolewa jana (Novemba 13, 2019) imewataka wanafunzi wote wa taasisi za elimu ya juu ambao wanataka kukata rufaa kuziwasilisha kwa njia ya mtandao.
Dirisha la kuwasilisha rufaa hizo liko wazi kuanzia Novemba 13 had 23, 2019 na linapatikana kupitia http.olas.heslb.go.tz ambapo baada ya muda huo kupita wanafunzi watakaokua wametimiza masharti na sifa watapangiwa mikopo.
Ili kuwasilisha taarifa na nyaraka za rufaa, mwanafunzi anapaswa kufungua mtandao huo, kusoma maelekezo na kutumia namba yake ya mtihani wa kidato cha nne aliyoombea mkopo kwa mwaka huu (2019/2020) kuingia na kuwasilisha taarifa zake kwa njia ya mtandao tu.
Novemba 10,2019, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hadi kufikia Novemba 3, mwaka huu, Serikali imekwishatoa mikopo ya sh. bilioni 162.8 kwa wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza nchini kote.
“Kwa mwaka 2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 450 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi walengwa 128,285.
“Na hadi tarehe 3 Novemba, 2019 wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka 2019/2020, walikuwa wamepewa mikopo inayofikia shilingi bilioni 162.8,” alisema Majaliwa wakati akizungumza na maelfu ya waumini waliohudhuria Baraza la Maulid kitaifa katika viwanja vya Benki Kuu (BoT) Capripoint, jijini Mwanza.
- Waombaji 30,675 Heslb wapata mkopo elimu ya juu awamu ya kwanza
- HESLB kutoa majina waliopata mikopo awamu ya kwanza Oktoba 17
Mikopo hiyo huwasaidia wanafunzi waliopo vyuoni kujikimu na kugharamia mahitaji ya masomo ikiwemo ada ya mwaka.
Hata hivyo, siyo wote wanapata mikopo hiyo kutokana wingi wa wanafunzi.