July 5, 2024

HESLB yaongeza siku 10 kwa waombaji mikopo Tanzania

Uamuzi huo unafuatia maoni, ushauri na maombi kutoka kwa wanafunzi, wazazi na walezi ambayo HESLB imeyapokea.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru (katikati) akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari leo Jumatatu (Agosti 31, 2020) kuhusu kuongezwa kwa muda katika dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu katika mwaka wa masomo 2020/21. Kushoto ni Meneja Masoko wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Joseph Kimaro na kulia ni Meneja Mkuu Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mwanaisha Said. Picha| HESLB.


  • Bodi hiyo ya mikopo imeongeza muda wa siku 10 za kuomba mkopo kuanzia kesho Septemba 1, 2020.
  • Uamuzi huo unafuatia maoni, ushauri na maombi kutoka kwa wanafunzi, wazazi na walezi ambayo HESLB imeyapokea.
  • Wanafunzi 54,000 wa mwaka wa kwanza kupata mikopo hiyo 2020/21. 

Dar es Salaam. Ikiwa wewe ni miongoni mwa wanafunzi ambao wanatarajia kujiunga na elimu ya juu mwaka huu na bado hujafanikiwa kutuma maombi ya mkopo katika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), basi neema imekushukia kwa sababu una siku 10 za ziada kukamilisha zoezi hilo. 

Mkopo wa elimu ya juu huwasaidia wanafunzi waliopo katika vyuo mbalimbali nchini Tanzania kupata fedha ya kujikimu na ada kwa ajili ya masomo kila mwaka. 

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema bodi hiyo imeongeza muda wa siku 10 za kuomba mkopo kuanzia kesho Septemba 1, 2020 ili kuwawezesha wanafunzi ambao bado hawajafanikiwa kutuma maombi, wafanye hivyo kwa muda uliobaki.

Badru aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es salaam leo (Agosti 31, 2020) amesema uamuzi huo unafuatia maoni, ushauri na maombi kutoka kwa wanafunzi, wazazi na walezi ambayo HESLB imeyapokea.

“Mwisho ilikua iwe leo saa sita usiku, lakini tumeamua kuongeza siku 10 ili kuwawezesha wateja wetu ambao hawajakamilisha maombi yao kufanya hivyo,” amesema Badru. 

Kwa mujibu wa Badru, tayari HESLB imeshapokea maombi ya mikopo zaidi ya 80,000 kutoka kwa waombaji ambao wengi wao ni wahitimu wa kidato cha sita ambao sasa wako katika mafunzo ya uzalendo katika kambi 18 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). 

“Hadi leo asubuhi, tumeshapokea maombi 85,921 kwa njia ya mtandao, na kati ya hayo, maombi 71,888 sawa na asilimia 84 ni kamilifu na yana nyaraka muhimu na mengine 14,033 yanakosa nyaraka muhimu kama vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi wa waombaji ambavyo havijathibitishwa na RITA au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar maarufu kama ZCSRA,” amesema Badru.


Zinazohusiana: 


Katika mwaka wa masomo 2020/21, Serikali imetenga Sh464 bilioni kwa ajili ya wanafunzi 145,000 wa taasisi za elimu ya juu na kati yao, 54,000 wanatarajiwa kuwa ni wa mwaka wa kwanza.

Kuhusu malipo kwa wanafunzi waliopo vyuoni, Badru amesema Sh15.57 bilioni zimetumwa vyuoni kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi 39,721 wanufaika kuendelea na mafunzo kwa vitendo katika maeneo mbalimbali kuanzia wiki hii.

Katika mwaka wa masomo wa 2019/2020, Serikali ilitenga Sh450 bilioni kwa ajili ya mikopo ambazo zimewanufaisha wanafunzi 132,292.

Ili kufanikisha maombi ya mikopo mwaka huu,  Meneja Mkuu anayesimamia Uendeshaji Biashara wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Mwanaisha Said amesema wamekubaliana na HESLB kuendelea kupokea nakala ngumu za maombi ya mikopo katika ofisi za TPC nchini kote na kuziwasilisha HESLB hadi Septemba 15 na kuwataka wanafunzi kutokuwa na wasiwasi wa kutokupokelewa kwa bahasha zao.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe ameitaka HESLB kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanafunzi waliowasilisha maombi yao yanafanyiwa kazi kwa wakati ili wapate mikopo hiyo.