November 24, 2024

Heslb yatakiwa kutoa mikopo kwa wanafunzi waliosomeshwa kwa ufadhili

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwapa mikopo wanafunzi wote ambao walikua wakisoma shule binafsi kwa ufadhili.

  • Aitaka Bodi ya mikipo kuwapa mikopo wanafunzi wote ambao walikua wakisoma shule binafsi kwa ufadhili.
  • Amewataka wanafunzi hao kuwasiliana na Bodi ili waweze kusaidiwa.
  • Agizo kama hilo alilitoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Agosti 10, 2019.

Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuwapa mikopo wanafunzi wote ambao walikua wakisoma shule binafsi kwa ufadhili.

Waziri huyo amesema kumejengeka dhana ya wanafunzi wanaosoma shule binafsi hawana uhitaji wa kupata mikopo kwa sababu wazazi au walezi wana uwezo wa kuwasomesha. 

Prof. Ndalichako ametofautiana na dhana hiyo na kusema siyo sahihi kwani wapo wanafunzi wanaosomeshwa na watu binafsi au wadhamini mbalimbali zikiwemo taasisi za kidini. 

“Naomba niwahakikishie kuwa Serikali inatambua watoto hawa ambao wanasomeshwa katika shule binafsi hivyo wanapojiunga na elimu ya juu watapatiwa mikopo ila wanatakiwa kuzingatia kujaza maelezo yao vizuri kwenye fomu ya mikopo,” amesema Prof. Ndalichako.


Zinazohusiana


Ametoa agizo hilo jana (Septemba 22, 2019) jijini Dar es Salaam, wakati akifungua wiki ya elimu na kituo cha kulelea watoto wanye uhitaji katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), usharika wa Kimara.

Katika kuhakikisha wanafunzi hao hawapishani na fursa hiyo, amewataka wanafunzi ambao walikuwa wamewasilisha fomu za maombi ya mikopo bila kujaza taarifa za ufadhili kuwasiliana na bodi hiyo ili waweze kuongezea taarifa hizo.

“Kama wapo ambao walishindwa kujaza vyema maelezo yao, bodi bado inaendelea na usajili ni muhimu wakaenda kuomba kufanya marekebisho wajaze taarifa hizo kwa usahihi ili waweze kunufaika na mikopo,” amesema.

Agizo kama hilo liliwahi kutolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita ambapo aliitaka Bodi hiyo kutafakari utoaji wa mikopo kwa wanafunzi waliosoma shule binafsi.

Majaliwa alisema wapo wanafunzi wanaofaulu vizuri kidato cha nne na kukosa nafasi katika shule za Serikali na kutokana na kutoka katika familia zisizokuwa na uwezo, wengi wao hutafuta wafadhili na kusoma kwenye shule binafsi.