November 24, 2024

Hifadhi za jamii zinazosubiri wawekezaji Tanzania

Ni ikona iliyopo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Enduimet iliyopo karibu na Mlima Kilimanjaro.

Uwekezaji katika maeneo yenye tija. Picha| Mtandao.


  • Ni ikona iliyopo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Enduimet iliyopo karibu na Mlima Kilimanjaro. 
  • Zimesheni vivutio vingi vya utalii vinavyohitaji uwekezaji. 

Dar es Salaam. Tanzania imebarikiwa kuwa na maeneo mengi ya asili ambayo yakiendelezwa yanaweza kutumika kuiingiza nchi mapato na kuwafaidisha wananchi wake. 

Hifadhi za jamii ambazo ziko chini ya usimamizi wa wanyama pori ni miongoni mwa maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wanaoweza kujenga hoteli na kutoa huduma mbalimbali za utalii. 

Kama bado una ndoto ya kuwekeza katika sekta ya utalii, basi hifadhi za jamii za Ikona na Enduimet zinaweza kuwa maeneo muhimu ya yatakayokufungulia fursa za kutengeneza kipato. 

Ikona

Hifadhi ya jamii ya Ikona ipo katika Wilaya ya Serengeti ikipakana na hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika kijiji cha Robanda kwa upande wa kaskazini mashariki ikiwa imepakana na pori la akiba la Ikorongo.

Eneo hilo  lenye ukubwa wa kilomita za mraba 242.3. Linapatikana kilomita 270 kutoka uwanja wa ndege wa Arusha ambapo ni eneo kuu la kuingilia na kutokea linalotumika na watalii.

Vivutio vilivyopo katika eneo hilo ni pamoja na mapori ya akiba mawili ya Ikorongo na Grumeti, inayofanya eneo hilo kuvutia kwa sababu ya idadi kubwa ya wanyama ambao wanapatikana pia katika Serengeti.


Zinazohusiana.


Enduimet 

Hifadhi ya Jamii ya Enduimet ipo magharibi mwa mkoa Kilimanjaro, Wilaya ya Longido ambapo upande wa kusini mashariki imepakana na hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.

Eneo hilo linaweza kufikiwa kupitia Boma Ng’ombe au Sanya juu au barabara ya kutokea Arusha kwenda Namanga wilaya ya Longido kwenda Sinya.

Enduimet ni eneo linalochukua kilomita za mraba 1,282. Enduimet ni kiunganishi cha kufika katika mbuga za wanyama za Amboseli na Kilimanjaro, eneo hilo lililo sheheni mimea mbalimbali imepelekea kua na wanyama tofauti waliomo hapo na kutengeneza makazi katika eneo hilo.

Wanyama kama viboko, twiga, tembo, pundamilia, chui na wanyama wengine wengi. Ndani ya eneo hilo kabila la wamaasai wamepata eneo maalum la kutulia kutokana na shughuli wanazofanya zinazohusu uchungaji.

Shughuli nyingi zinaweza kufanyika katika maeneo hayo kutegemea na asili ya eneo lenyewe ni pamoja na utalii kwa kuchukua matukio ya picha ndani ya maeneo hayo, mbio za mamorani na utalii wa kitamaduni.