October 6, 2024

Hifadhi za Taifa unazoweza kuzitembelea kidijitali kwenye simu yako

Huenda hii ikawa ni habari njema kwako kwani katika pita pita zangu, Nimekutana na tovuti ya sanaa na tamaduni iliyo chini ya kampuni ya teknolojia ya Google ambayo imenipeleka sehemu tatu tofauti za utalii kwa kutumia simu yangu ya mkononi.

  • Google wameanzisha tovuti inayotumia mfumo wa 360 kukuwezesha kufanya utalii ukiwa popote ulipo kwa kutumia simu yako.
  • Kwa sasa unaweza kutembelea hifadhi tano za Marekani ikiwemo ya Huwai’i Volcano. 
  • Kuzifikia hifadhi hizi, unahitaji bando ya kutosha na mtandao unaoeleweka.

Dar es Salaam. Kama ilivyo hali yangu kwa sasa na hali ya kila anayependa kutembelea vivutio vya utalii.  Huenda unatamani kusafiri lakini pochi yako, mlipuko wa virusi vya Corona haziruhusu kufanya hivyo.

Bahati yao ambao wanapenda kuangalia filamu kwani mtandao wa kuangalizia filamu wa Netflix hakika unawabeba na hata wale ambao wanapenda muziki basi hakika mitandao ya Youtube, Spotify na mingineyo ipo katika upande wao. Mambo yote ni mwendo dijitali tu.

Mimi na wewe ambao tunapenda kutalii tunabaki na nani? 

Huenda hii ikawa ni habari njema kwako kwani katika pita pita zangu, Nimekutana na tovuti ya sanaa na tamaduni iliyo chini ya kampuni ya teknolojia ya Google ambayo imenipeleka sehemu tatu tofauti za utalii kwa kutumia simu yangu ya mkononi.

Ndiyo! Ndani ya siku moja, nimetembelea sehemu tatu tofauti ikiwemo ile ambayo nimekuwa nikipenda kwenda baada ya kusikia sifa zake, hifadhi ya Taifa ya Hawai’i Volcano iliyopo nchini Marekani.

Hizi ndizo hifadhi ambazo unaweza kuzitembelea kidijitali ukiwa kwenye kochi, kiti kitanda na nani anajua? Hata kwenye nyasi nyumbani kwako:

Hifadhi ya Taifa ya Huwai’i Volcanoes 

Hifadhi hii ipo kwenye visiwa vya Hawaii nchini Marekani. Hakika utakuwa umesikia mengi kuhusu Hawaii lakini bado hujajua mengi yaliyomo ndani yake.

Hifadhi hii ambayo imeshikilia historia kubwa ya visiwa hivyo, itakuacha mdomo wazi kwa upekee na uzuri wake.

Kupitia teknolojia ya nyuzi 360 iliyotumika katika kutengeneza utalii huo wa kidijitali, unaweza hadi kushuhudia kilele cha mlima Halema’uma’u ndani ya hifadhi hiyo. Zaidi, unaweza kupasua anga na kuona kina cha mlima huo wenye volcano hai, kusikiliza sauti na muungurumo wa lava na hata kupata simulizi ya mambo yaliyopita.

Niliyafanya hayo yote nikiwa kwenye kiti changu.

Safari yangu iliendelea hadi kwenye kapeti ambapo nilijilaza na kujikuta kwenye hifadhi nyingine.

Hifadhi ya Volcanoo ya Hawaii huwa na muonekano mpya kila baada ya mlipuko wa valcano. Picha| Wandering wagers.

Hifadhi ya Taifa ya Carlsbad Caverns

Hifadhi hii iligunduliwa miaka 120 iliyopita jijini New Mexico nchini Marekani baada ya kundi la popo kuonekana wakitokea kwenye pango hilo ambalo sasa ni utalii unaokupeleka futi 120 chini ya ardhi ukikuacha na mshangao juu ya muda uliotumika kutengeneza uzuri huo.

Kupitia simu ya mkononi, unaweza kuiona hifadhi hii huku ukifanya hata yale yasiyowezekana, yaani kupaa na popo wanaoishi kwenye mapango ya hifadhi hiyo.

Hifadhi hiyo yenye mapango zaidi ya 100 itakustaajabisha kwa namna mapango na miamba ya hifadhi hii ilivyotengenezwa huku pango lenye ukubwa zaidi ya viwanja sita vya mpira wa miguu likikusubiri ulitazame.

Hifadhi ya Bonde la Bryce 

Hifadhi hiyo inayopambwa na upekee wa rangi nyekundu na za machungwa, ni kati ya hifadhi zenye jangwa nchini Marekani unazoweza kuzifikia huku ukiwa jikoni kwako unapika au chumbani.

Uzuri huo uliojificha kwenye ardhi yenye ukubwa wa kilometa za mraba milioni 1.45 ni kati ya sehemu ambazo nchi ya Marekani inajivunia huku watalii wakizidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.


Zinazohusiana


Hifadhi ya Taifa ya Tortugas

Hifadhi hii ni hifadhi ya majini yenye visiwa saba. Kwenye hifadhi hii utaona jinsi utalii wa uvuvi unavyofanyika, kupiga mbizi na aina zingine za burudani. Inapatikana Florida nchini Marekani.

Hata hivyo, hauwezi kuogelea ukiwa unaiona kwenye mtandao lakini bado utafurahia uzuri adimu ukionekana kwenye simu yako.

Sauti za masimulizi kutoka kwa kiongozi wa safari yako anayetumia bando lako tu kukuelekeza zitakuacha ukiwa na ufahamu kana kwamba umetembelea nchi ya Marekani bila hata kupata visa.

Hifadhi ya Taifa ya Kenai Fjords

Hifadhi hii ipo kwenye jiji la Alaska nchini Marekani ambayo imezungukwa na maji na vivutio vingine kede kede.

Furahia safari za boti huku muonekano wa miamba barafu ukiwemo mwamba Exit ambao unaonekana kwa urahisi hata ukiwa barabarani. 

Ajabu ya kwamba sehemu zote hizo unaweza kuzifikia ukiwa umekaa na familia yako hasa kipindi hiki cha janga la virusi vya Corona.

Bado unahitaji kupata furaha, usiruhusu Corona ikuharibie mipango yako. Fanya utalii wa kidijitali.