Hii ndiyo filamu inayoweza kulipa nguvu penzi lililochacha
Ni filamu ya “The Wrong Missy” inayosimulia kisa cha mtanashati anayekosea kutuma ujumbe unaomfikia mwanadada ambaye amekuwa akimkwepa.
- Ni filamu ya “The Wrong Missy” inayosimulia kisa cha mtanashati anayekosea kutuma ujumbe unaomfikia mwanadada ambaye amekuwa akimkwepa.
- Wawili hao ambao kwa Morris haoni kama wanaendana, wanasafiri wote kula bata visiwa vya Hawaii.
- Mdogo mdogo, upele unapata mkunajji baada ya Morris kuona upande wa tofauti wa binti Missy.
Dar es Salaam. Kila mwanaume ana mwanamke wa ndoto zake. Ndiyo! Yule mlimbwende ambaye huenda amemuona kwenye filamu au kwenye moja ya sehemu alizowahi kuzitembelea.
Kwa Tim Morris (David Spade), mrembo wa ndoto zake anakutana naye kwenye uwanja wa ndege akiwa kwenye shughuli zake za safari.
Kama filamu la Kihindi, wanagongana, vitu vinaanguka, wakiinama kuviokota na kuonana, tabasamu linashamiri kati yao kiasi cha kuufunika mwangaza wa jua.
Naam! Penzi kwa muono wa kwanza yaani “love at first sight” ukitaka kutumia lugha uliyopanda “school bus” ili kuisoma.
Morris ambaye ni mfanyakazi kwenye kampuni mashuhuli anapata bahati ya mtende baada ya kufanikiwa kuonana na mrimbwende Melissa (Molly Sims) na anazidi kuwa hoi baada ya mrembo huyo aliyewahi kunyakua taji la urimbwende kusema “huu ni wakati mzuri nimepata na mwanaume ambao sijaupata kwa muda mrefu sana.”
Kama zali la mentali, inatokea safari ambayo kampuni anayofanyia kazi Morris imeandaa na unajua nini? Unaruhusiwa kwenda na mpenzi wako.
Kwa haraka Morris anainua simu yake kwa dhamira ya kumtafuta Melissa ili amuombe kuambatana naye kutembelea kisiwa cha Hawaii.
Zinazohusiana:
- Unafikiri kila mapenzi ni mahaba? Filamu ya “The Half of It” ni tofauti
- Hivi ndivyo mali inavyoweza kumbadilisha binadamu mwenye moyo wa malaika
- Muujiza uliotokea chumba namba saba gerezani
Hata hivyo, anaingia mkenge baada ya ujumbe huo kwenda kwa mwanadada mwenye papara zake, mwenye jina Missy (Lauren Lapkus).
“Nina mwanadada anakuja hapa na ni bonge la toto,”ni maneno ya Morris akijitapa kwa jirani yake. Mshangao unajaa usoni baada ya Missy kuja badala ya Melissa.
Ni kitumbua kimeingia mchanga. Missy asiyejua maana ya staha na kujivunga mbele za watu, anabahatika kwenda Hawaii na mtu aliyekutana naye mara moja kwenye “kideti upofu” (blind date).
Mdogo mdogo, treni ya Moriss inaanza kuingia kwenye reli ya Missy ambaye hakutaka hata kumsikia, mahaba niue, nipondeponde ukiweza nizike yanashamiri kwenye filamu hii ya “The Wrong Missy” ambayo bado upya wake unafuka moshi kwenye mtandao wa Netflix ambao unalipiwa kwa mwezi kuanzia Sh18,489.
Ni bando lako tu litakayokuwezesha kutazama filamu hii ya mahaba yeye ucheshi iliyoongozwa na Tyler Spindel mwenye alama yake kwenye filamu za ucheshi zikiwemo za “Jack and Jill” na “Father of the Year”.