July 8, 2024

Hii ndiyo kazi inayoweza kukupatia furaha daima

Kwa kuzingatia kuwa unatumia takriban saa nane kwa siku ukiwa kazini, unahitaji kazia ambayo utaifurahia.

  • Ni kazi ambayo unafanya kwa kupenda na siyo kupata fedha.
  • Ni kazi ambayo inachangia kupata furaha na afya bora.

Dar es Salaam. Leo tufikirie kwa pamoja. Wewe unayesoma makala haya, unaipenda kazi unayofanya?

Wapo wanaofanya kazi ya ualimu kwa sababu bila kazi hiyo, mkono hauwezi kwenda kinywani. Wapo pia wanaofanya kazi ya udaktari kwa sababu ndiyo kozi waliyosomea huku wengine wakifanya kazi za upishi kwa sababu ndiyo kitu pekee wanachokimudu.

Wakiwa makazini, wengi husubiri muda wa kutoka kazini ili warudi majumbani kwao kuingoja asubuhi ili waamke wakateseke upya kesho yake. Hao wamechagua kazi badala ya furaha yao.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliamua kufanya wanachokipenda na hivyo wamechagua furaha badala ya kazi zao. Wengi wao husema wamechagua uhuru, amani na kuchukua uskani wa maisha yao.

Kama unafanya kazi ambayo huipendi basi jiandae kwa haya:

Hautafanya kazi hiyo kwa ufanisi

Umewahi kukuta kazi ya ujenzi iliyofanywa na mtu ambaye hafurahii kazi hiyo? Ukuta kupinda, nyumba kukaa upande upande na mengine kama hayo.

Kwa mtu anayefurahia kazi yake akiwemo Undare Mtaki ambaye ni mchoraji wa picha za rangi jijini Dar es Salaam, kuna namna ambavyo kazi yake lazima itakuvutia kwa kuitazama.

Mtaki ambaye amesomea masuala ya usanifu wa majengo anasema licha ya kuwa anaipenda taaluma yake, amani yake ipo kwenye uchoraji ambao humpatia furaha ya moyoni.

Kijana huyo ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kwa mapenzi aliyonayo katika uchoraji, anaweza kuchora picha moja kwa ustadi hata kama ichukue miezi mitatu.

Kwa Mtaki, Uchoraji wake unaongezewa nakshi na taaluma yake ya usanifu na hivyo kutengeneza kazi yenye ubora wa hali ya juu.

Kwa upande mwingine, wapo ambao hufanya kazi kwa sababu ya pesa hivyo hawawezi kuweka umakini wote katika kuona uzuri wa matokeo ya kazi walizozifanya.

Kama unatumia takriban saa nane kwa siku ukifanya kitu ambacho hukipendi, kuna amani gani katika maisha yako? Picha| Freepik.

Msongo wa mawazo

Kuna tofauti kati ya kufanya kazi ili usubirie malipo yako mwisho wa mwezi, wiki na kadhalika na kufanya kazi ili uendelee kuwa bora katika unachokifanya.

Moja ya rafiki zangu, Rogers Mugisha ambaye  ni mbunifu wa programu aliwahi kuniambia kuwa mara kadhaa hujikuta akifanya kazi hadi saa saba za usiku bila kuchoka na muda mwingine, anakua anaona kama muda haujamtendea haki kwa kupeleka saa mbele kwa haraka.

Kinachompa mawazo Mugisha katika kazi yake ni kuwa bora kila siku na hivyo kumpa motisha ya kuendelea kuifanya kazi yake huku akijinoa.

Mugisha ni tofauti na mmoja ya rafiki zangu ambaye  anafanya kazi katika idara ya mawasiliano ya moja ya makampuni ya kutoa huduma za simu.

Rafiki huyo ambaye nitamuita Timana ili kulinda ajira yake, kila siku analalamika muda unaenda taratibu na anatamani kutoka mapema kazini.

Timana anafanyia kazi mshahara wake lakini hana furaha na kazi yake, jambo ambalo linampa msongo wa mawazo juu ya hatma ya maisha yake.


TANGAZO


Ni mwanzo wa kuchokoza afya ya akili yako

Afya ya akili inahitaji vitu vingi ikiwemo kuepuka ama kupunguza matumizi ya madawa ya kulevya, matumizi ya pombe na kushindwa kutatua changamoto za kimaisha mapema.

Changamoto za kimaisha zinaweza zikasababishwa na kazi yako ikiwemo kukosa muda wa kupumzika, msongo wa mawazo na kwa baadhi hali hiyo huwatumbukiza kwenye unywaji wa pombe na kutumia dawa za kulevya.

Kwa mujibu wa mtaalam wa masuala ya fedha, Edmund Munyagi, kufanya kazi ambayo hauipendi kwa maisha yako yote haitokupatia afya njema ya akili kutokana na kukosa amani kwa muda mrefu na mawazo yasiyoisha.

“Wapo watu wanaopata kipato kidogo lakini wana amani nyumbani kwao na furaha na wale wanaopata fedha nyingi lakini furaha hawana,” anasema Munyagi.

Mtaalamu huyo wa masuala ya fedha anasema kwa baadhi furaha inaweza kuwa kwenye kazi yao na mara nyingi watu hao hawaoni kufanya kazi ni mateso.

Baadhi ya watu huishia kutumbukia kwenye ulevi na matumizi ya madawa ya kulevya kutokana na msongo wa mawazo unaochochewa na kazi wanayoifanya. Picha| Freepik.

Ni muhimu kufahamu kuwa pesa ina sehemu ya kuleta furaha katika maisha haya lakini pia furaha inatokana na kazi unayofanya.

Mwandishi wa vitabu na mwamasishaji wa vijana, Neema Simbo anasema watu wengi wanafikiri kuwa furaha ni kuwa na pesa hivyo wapo tayari kupitia mateso ya siku 30 kila mwezi kufurahi siku ambapo mshahara wao utaingia.

“Tumeingia duniani bila pesa na tutaondoka bila pesa pia. Kuna mambo mengi ya kukupatia furaha ikiwepo marafiki, familia na kipaji chako,” amesema Simbo.

Swali ambalo bado ninabaki kujiuliza ni je, rafiki na ndugu na familia watanipenda hata nikiwa sina pesa ambayo ni furaha kwa wengi? Wewe unadhani furaha ipo wapi?

Tukutane wiki ijayo katika makala hizi za njiapanda.