October 6, 2024

Hoteli zaanza kufungwa kuepuka Corona Tanzania

Baadhi ya hoteli maarufu na ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu wengi nchini Tanzania zimeanza kufungwa ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona ambavyo vinaitesa dunia kwa sasa.

  • Hoteli ya Sea Cliff ya jijini Dar es Salaam itafungwa ifikapo Aprili 1, 2020.
  • Hoteli zingine zasitisha baadhi ya shughuli ikiwemo migahawa ya chakula. 
  • Wananchi watakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo.

Dar es Salaam. Baadhi ya hoteli maarufu na ambazo zimekuwa zikitumiwa na watu wengi nchini Tanzania zimeanza kufungwa ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya Corona ambavyo vinaitesa dunia kwa sasa. 

Virusi hivyo aina ya COVID-19 mpaka jana (Machi 27, 2020) kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) vimeambukiza watu 509,164  na 23,335 wamefariki kutokana na maradhi hayo duniani.

Uongozi wa hotel ya Sea CLiff Court ya Jijini Dar es Salaam inayomiliki hoteli na nyumba za kulala wageni (Apartments) umetangaza kufunga kwa muda shughuli zake zote ifikapo Aprili 1, 2020. 

Taarifa ya hoteli hiyo inaeleza kuwa kutokana na mazingira na athari za ugonjwa wameamua kuchukua maamuzi ya kimkakati yatakayotekelezwa katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huo.

“Ingawa ni huzuni lakini maamuzi haya lazima yatekelezwe, tunafahamu kuwa yataathiri wasambazaji, wateja na wafanyakazi wetu,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo. 

Uongozi wa hoteli hiyo umesema unaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya ugonjwa huo na hali ikitengamaa wanatafungua tena hoteli hiyo na nyumba za wageni ambazo ziko Masaki katika jiji hilo ambalo limethibitika kuwa na visa vya wagonjwa nane mpaka sasa. 

“Asanteni sana kwa uelewa wenu kuhusu suala hili,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ya hoteli ya nyota tano ambayo hutembelea na watu maarufu. 

Hata hivyo, hoteli ya Sea Cliff ya Zanzibar imeiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa inaendelea na shughuli zake kama kawaida na ikitokea wanataka kusitisha watatoa taarifa kulingana hali ya ugonjwa wa Corona.

Nayo hoteli ya Serena imetangaza kufunga shughuli za hoteli na makambi yake katika nchi za Kenya na Tanzania mpaka Juni 15 wakati ikiendelea kutafakari namna ya kuendesha biashara yake barani Afrika. 

Nchini Tanzania, matawi ya hoteli zilizofungwa ni pamoja na zile zilizopo katika hifadhi za Taifa za Ziwa Manyara, Serengeti na Ngorongoro. Kambi zilifungwa ni Kirawira na Mbuzi Mawe.

Moja ya hoteli za kifahari za Serena ambazo sasa zinachukua hatua ya kuwakinga wateja wake na virusi vya Corona. Picha| PADERBORNERSJ

Kwa upande wa Kenya, Serena imefunga matawi yake yaliyopo katika Hifadhi za Taifa za Amboseli, Kilaguni, Mara na hoteli ya Serena mountain Lodge huku kambi ya Ziwa Elmenteita iliyopo kilomita 120 Kaskazini Mashariki mwa jiji la Nairobi. 

“Maamuzi hayo yatabadilisha ikiwa mipaka ya nchi itafunguliwa na hali ya soko itakaporejea katika hali yake, jambo ambalo tumekuwa tukilitazamia,” amesema Mahmud Jan Mohamed, Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli za Serena Afrika katika taarifa yake. 

Hoteli zingine zachukua hatua

Hoteli mbalimbali nchini Tanzania zimechukua hatu kuwalinda wateja na wafanyakazi wake wakati wakitumia maeneo ya kulala na kupata chakula. 

Hoteli za White Sands na Double Tree za Jijini Dar es Salaam zimewataka wateja wake kuzingatia miongozo ya kiafya inayotolewa na mamlaka za afya na  wateja wao wanapaswa kuwasiliana nao kabla ya kuweka oda ya kukaa katika hoteli hizo.


Soma zaidi:


Nayo hoteli ya Hyatt Regency iliyopo Posta jijini hapa, imeeleza kuwa baadhi shughuli katika migahawa yake zitakuwa na huduma chache ikilinganishwa ilivyokuwa awali. 

Hatua hizo zilizochukuliwa na hoteli za Tanzania, pia zimechukuliwa na hoteli zingine katika mataifa yaliyoendelea ambako ugonjwa huo umeathiri watu wengi.

Mathalan, Hoteli ya Sarova nchini Kenya imesitisha shughuli zake zote katika matawi yake manne ya Sarova Woodlands Hotel & Spa iliyopo Nakuru, Sarova Lion Hill Game Lodge (Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Nakuru),  Sarova Mara Game Camp (Pori la Akiba la Masai Mara) na Sarova Taita Hills Game Lodge,  iliyopo katika mbuga ya wanyama ya Taita Wildlife Sanctuary iliyopo katika kaunti ya Taita-Taveta.