Hujuma za namna hii zikomeshwe
Ni za uharibifu wa miundombinu ya umeme ambazo zinafanywa na watu wenye nia ovu.
- Ni za uharibifu wa miundombinu ya umeme ambazo zinafanywa na watu wenye nia ovu.
- Hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu wanaowakosesha watu kupata umeme wa uhakika.
Nichukue fursa hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutupigania hasa kwa nyakati hizi zenye magonjwa ya ajabu kama huu wa COVID-19 uloenea dunia nzima na kusababisha taharuki kubwa bila kujali uwezo wa nchi kiuchumi iwe imeendelea au inaendelea.
Pili, niseme kwa masikitiko makubwa kuhusu kitendo cha kuangusha nguzo kubwa yenye kuimarisha usambazaji wa nyaya za kupeleka huduma ya umeme makao makuu ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Hujuma hii ilifanyika Mei 30, 2020 na kusababisha makao makuu ya wilaya Mlele kukosa huduma ya umeme hadi mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) waliporejesha huduma hiyo Mei 31, 2020.
Sehemu ya Nguzo ya umeme iliyokatwa na kuanguka ikiwa juu ya msitu katika Wilaya ya Mlele. Picha| Ernest Kanumba.
Hujuma hiyo ya kuangusha nguzo ya umeme ilitokea katika eneo kati ya Uzega na Inyonga wilayani Mlele.
Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya Watanzania ambao hawana mapenzi mema kwa nchi yao wanahujumu juhudi za kitaifa za kuliletea maendeleo endelevu Taifa kwa nishati ya umeme.
Ni vigumu kuamini kuwa pamoja na jitihada zote zinazofanywa na Serikali, baadhi ya watu wanadiriki kuhujumu kazi ya kuwapelekea wananchi umeme.
Kitendo cha kukata na kusababisha nguzo ya umeme ianguke chini ni uuaji uchumi wa nchi yetu kwa sababu jitihada za Serikali kupeleka umeme vijijini na mjini inaendelea kwa kasi.
Kuzalisha na kusambaza umeme ni gharama kubwa sana lakini wahujumu hilo hawalioni bali wako tayari kufanya wapendavyo ili mradi haja zao zitimizwe kwa gharama yoyote ile.
Hujuma kama hizi si za kufumbia macho. Lazima zikemewe na kulaaniwa na wote wenye nia njema kwa maendeleo ya Taifa hili.
Binafsi sijafurahishwa na kitendo hiki na naamini vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, vitawasaka na hatimaye kuwakamata wahusika na kuwafikishwa mahakamani.
Dk Felician Kilahama ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki mstaafu Tanzania.