July 1, 2024

Huu ndiyo mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan amesema dira na muelekeo wa Serikali ya awamu ya sita anayoingoza ni kudumisha mambo yaliyofanywa katika awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.

  • Ni kudumisha mambo yaliyofanywa katika awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.
  • Baadhi ya mambo yatabadilishwa ili kuongeza ufanisi wa Serikali.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema dira na muelekeo wa Serikali ya awamu ya sita anayoingoza ni kudumisha mambo yaliyofanywa katika awamu zilizopita, kuyaendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza leo Aprili 22, 2021 jijini Dodoma wakati akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais Machi 19 mwaka huu amesema yapo baadhi ya mambo yatabadilishwa ili kuongeza ufanisi wa Serikali.

“Dira na muelekeo wa Serikali  ya awamu ya sita ni kudumisha mazuri ya awamu zilizopita, kuendeleza mema yaliyopo na kuleta mengine mapya. Hii ndio dhana na maana halisi ya kauli mbiu au salamu yetu ya “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi iendelee,” amesema Rais Samia mbele ya Wabunge wa Bunge la Tanzania. 

Amesema mipango mbalimbali inayotekelezwa na awamu ya sita ni ile iliyokuwepo awamu ya tano iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu. 


Soma zaidi:


Amesema mipango hiyo itaongozwa na Dira ya Maendeleo ya 2025, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020/25, mpango wa 3 wa maendeleo wa miaka mitano, agenda ya maendeleo ya Afrika ya 2063 na agenda ya dunia ya malengo endelevu ya 2030.  

“Kwa kuwa nilivyowahi kusema huko nyuma, nirudie tena kuwa mimi na Hayati Dk Rais John Magufuli tulikuwa kitu kimoja. Kwa maana hiyo mambo mengi ambayo Serikali imepanga kuyatekeleza ni yale ambayo yalielezwa na Rais Hayati John Magufuli wakati akilizundua bunge hili,” amesema Rais Samia. 

Amesema Serikali inayoingoza itaelekeza nguvu kubwa katika kusimamia ukuaji wa uchumi, kudumisha amani na utulivu na kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara ili kuwezesha shughuli za biashara na utoaji huduma za kijamii.