Ifahamu nyumba ya mazalia ya nyuki hifadhi ya jamii Ipole
Ina mandhari nzuri ya upepo kutokana na miti na maliasili mbalimbali zilizopo katika eneo hilo kwa ajili ya utalii na uzalishaji wa asali.
- Ina mandhari nzuri ya upepo kutokana na miti na maliasili mbalimbali zilizopo katika eneo hilo.
- Ni eneo linalosifika kwa ufugaji wa nyuki.
- Pia ni sehemu nzuri kwa shughuli za utalii wa wanyama pori.
Dar es Salaam. Huenda bado unawaza ni eneo gani unaweza kuwekeza pesa zako katika shughuli za utalii na uzalishaji wa asali?
Hifadhi ya Jamii ya Ipole iliyopo Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora ni mahali sahihi kwa shughuli za utalii na uwekezaji wa uzalishaji wa asali unaoweza kukutoa kimaisha.
Inapakana na misitu ya Ipembambazi kwa upande wa mashariki na upande wa kusini inapakana na pori la akiba la Inyonga.
Ipole ni miongoni mwa hifadhi za jamii zinazopatikana Tanzania ikiwemo Mbomipa, Ikone, Randileni na Enduimet yenye mandhari nzuri kwa ajili ya shughuli za utalii.
Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Eneo hilo lina sifa ya kua na pori kubwa kwa ajili ya ufugaji wa nyuki, ikiwa na mandhari nzuri ya upepo kutokana na miti na maliasili mbalimbali zilizopo katika eneo hilo.
Zinazohusiana:
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
- Mauzo ya asali nje ya nchi yaongezeka zaidi ya mara nne, nta ikishuka
- Karafuu yachangia kushuka kwa mauzo ya nje Zanzibar
Eneo hilo ni makazi ya wanyama mbalimbali kama simba, twiga, tembo, ngedere na wanyama wengine wengi wadogo wadogo waishio nchi kavu.
Kitu kinachoitofautisha na maeneo mengine ni kuwa linafikika kirahisi na linafaa kwa uzalishaji wa asali na maliasili nyingine nyingi zinazofanya eneo hilo kuwa kivutio kwa watu wengi wanaotembelea mikoa ya Magharibi mwa Tanzania.
Shughuli mbalimbali zinazoweza kufanyika katika eneo hilo maalum la Ipole ni ufugaji wa nyuki pamoja na usimamizi wa maeneo mbalimbali ya akiba. Kama una mpango wa kuwekeza na fursa za biashara ya utalii ni Ipole.
Ipole ina mazingira mazuri kwa ajili uzalishaji wa asali. Picha|Mtandao.
Kwanini Ipole?
Eneo la hifadhi ya jamii ya Ipole lipo katika Wilaya ya Sikonge kilomita 96 kutoka Manispaa ya mkoa wa Tabora. Eneo hili lenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,540 limeundwa na vijiji vinne ambavyo ni Ipole, Msuva, Idekamiso na Itimula.
Kabla ya kuanzishwa kwa eneo hili hapo mwanzo miaka ya 1954 lilikuwa ni Pori la Akiba na eneo la hifadhi msitu wa Akiba.
Mnamo mwaka 2006, eneo hili lilitangazwa kuwa eneo la hifadhi ya jamii ya Ipole ili kuifanya jamii kushiriki kwenye uhifadhi wa wanyamapori na kupata faida za moja kwa moja kutokana na mapato ya shughuli za utalii zinapatikana kwenye hifadhi ya eneo hili.
Unaweza kufika katika eneo hilo kwa kutumia barabara ya Tabora mjini hadi Sikonge yenye kilomita 87 ambapo kutoka Sikonge hadi Ipole ni kilomita 24.
Pia unaweza kufika Ipole kwa kutumia barabara ya Mbeya Kitunda kwenda Ipole na pia unaweza kupitia Wilaya ya Mpanda (Katavi) hadi Iyonga kwenda Ipole.