Ijue mito mitano mikubwa Tanzania
Mito Ruvuma, Malagarasi, Kagera, Mara na Umba ndiyo mito mikubwa zaidi Tanzania.
- Mito Ruvuma, Malagarasi, Kagera, Mara na Umba ndio mito mikubwa Zaidi Tanzania.
- Inatumika kwa shughuli mbalimbali za uvuvi na kilimo.
- Pia ni kiungo muhimu cha Tanzania na nchi za jirani zikiwemo Msumbiji, Uganda, Burundi na Rwanda.
Dar es Salaam. Tanzania imebahatika kuwa na rasilimali nyingi za asili ikiwa ni pamoja na milima, maziwa, hifadhi za wanyama, mapori ya akiba, mito na mengine mengi yanaifanya kuwa na utajiri wenye kuvutia.
Kama ulikuwa hufahamu mito mikubwa iliyopo Tanzania, www.nukta.co.tz ipo kwa ajili ya kukuhabarisha na kukujulisha mito hiyo.
Uchambuzi wa ripoti ya Takwimu za Mazingira ya Taifa (National Environment Statistics Report, 2017) zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kuwa mito ya Ruvuma, Malagarasi, Kagera, Mara na Umba ndiyo mito mikubwa zaidi.
Mito hiyo inatumika kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uvuvi na kilimo lakini inatumiwa kama mipaka inayotenganisha Tanzania na nchi zingine.
5. Mto Mara
Kilomita 13,504 ndiyo ukubwa wa mto huu ukiwa ni mto wa tano kwa ukubwa nchini Tanzania. Mto Mara unapatikana katika nchi mbili za Tanzania na Kenya.
Chanzo chake kinaanzia katika nyanda za juu nchini Kenya na kutelemka hadi Tanzania katika mkoa wa Mara na kuishia katika Ziwa Viktoria lilipo katika mikoa ya Magharibi.
Mto huo hutumika zaidi na wafugaji kujipatia maji na malisho kwa ajili ya wanyama lakini pia hutumika na wanyama pori katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Ikorongo.
Zinazohusiana:
4. Mto Umba
Mto Umba ni mto unaopatikana kati ya Tanzania na Msumbiji na ukubwa wa kilomita 43,650. Upo kaskazini mashariki mwa Tanzania katika mkoa wa Tanga na unaenda kuishia nchini Kenya.
Chanzo chake kipo katika milima ya Usambara katika msitu wa Shagay na unatelemka kuelekea pwani ikipokea mito ya kando kutoka milima ya Usambara[, kilomita chache kabla ya kufika bahari ya Hindi unavuka mpaka wa Kenya kadi kaunti ya Kwale.
Mto huo ni kiungo muhimu kwa shughuli za utalii zinazofanyika katika mlima Usambara na Pori la Akiba la Umba.
3. Mto Kagera
Mto kagera ni mto wa tatu kwa ukubwa Tanzania wenye kilomita 59,800, unaopatikana Uganda, Rwanda, Burundi pamoja na Tanzania.
Mto huu unaanzia Burundi kuelekea kaskazini mpaka kati ya Tanzania na Rwanda na kugeukia mashariki karibu na mji wa Kikagati mpaka kati ya Tanzania na Uganda.
Sehemu ya mwisho ya njia yake inaingia kabisa ndani ya eneo la Tanzania hadi kufika Ziwa Victoria kaskazini mwa mji wa Bukoba.
Jina la mto wa Kagera limekuwa pia jina la mbuga ya wanyama ya Akagera huko Rwanda na pia jina la Mkoa wa Kagera nchini Tanzania.
Mto huu unaanzia Burundi kuelekea kaskazini mpaka kati ya Tanzania na Rwanda na kugeukia mashariki karibu na mji wa Kikagati mpaka kati ya Tanzania na Uganda. Picha|Mtandao.
2. Mto Malagarasi
Ni mto wa pili kwa ukubwa, una ukubwa wa kilomita 67,710. Unapatikana Burundi na magharibi mwa Tanzania huku ukitiririka hadi Ziwa Tanganyika.
Malagarasi huingia Tanzania upande wa mashariki wa Ziwa Tanganyika kilomita 40 kusini mwa Kigoma, karibu na Ilagala. Mto huo una matatwi mbalimbali kama mto Moyowosi na mto Nikonga.
Maji ya mto huo yanaingia Ziwa Tanganyika yanachangia maji ya mto Kongo na baada ya hapo bahari ya Atlantiki.
1. Mto Ruvuma
Huu ni mto wa kwanza kwa ukubwa nchini Tanzania, wenye ukubwa wa kilomita 152,200. Unapatikana Msumbiji pamoja na Tanzania. Chanzo cha mto huu kinapatikana mashariki mwa mji wa Songea katika milima ya Mitagoro upande wa mashariki wa ziwa Nyasa.
Unapofikia mpaka wa Tanzania na Msumbiji, takriban kilomita 200 baada ya chanzo, unageuka tena kuelekea mashariki hadi bahari. Kilomita 35 baada ya kuungana na mto Lujenda pana maporomoko ya Upinde.