November 24, 2024

Ijue njia bora ya kukabiliana na habari za uzushi kuhusu Covid-19

Ni mfumo wa “Flattening the curve” ambao mtu mmoja ana uwezo wa kuokoa mamia ya watu dhidi ya athari za habari za uzushi.

  • Ni mfumo wa “Flattening the curve” ambao mtu mmoja ana uwezo wa kuokoa mamia ya watu dhidi ya athari za habari za uzushi.
  • Ili kuwa shujaa, hakiki taarifa yako kabla ya kuituma kwa wenzio hata kama nia ni kuiokoa jamii.

Dar es Salaam. Baadhi ya watu husambaza habari pindi wanapoipata bila ya kuihakiki. Kitu ambacho hawakifahamu ni kuwa tabia hiyo ni hatari iwapo watasambaza habari za uzushi ambazo zina madhara makubwa kwa jamii. 

Mfano, mtu mmoja anapotuma ujumbe wa uzushi kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) kwenye kundi sogozi la mtandao wa kijamii wa WhatsApp na hata mitandao mingine, ujumbe huo hautaishia hapo. 

Baadhi ya watu watautuma ujumbe huo huo kwa wengine ili kufikisha ujumbe huo ambao huenda unaweza kupelekea hali ya taharuki iwapo utakuwa wa uzushi. 

Fikiria kama ujumbe wako umeutuma kwa watu 10 na hao watu kumi wakautuma kwa watu watano tu. Kwa maana hiyo, ujumbe huo utakuwa umewafikia watu 60 na wewe unakuwa mtu wa 61.

Kabla ya kutuma ujumbe wowote kuhusu ugonjwa wa COVID-19, jiulize kama ni ukweli na kama ujumbe huo umetolewa na chanzo cha kuaminika. 

“Kuwa chanzo cha kuushinda ugonjwa wa Corona, hakiki habari yako kabla ya kuisambaza ili kupunguza kasi ya kuusambaza (flattening the curve),” Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza katika mfumo wake mpya wa kudhibiti habari za uzushi za COVID-19. 

Shirika hilo linasisitiza kuwa usiisambaze habari ya ugonjwa huo iwapo huna uhakika nayo. 

“Kila siku, wote tunazungukwa na habari nyingi kuhusu COVID-19 na sio zote ni za kutegemewa,” imesomeka sehemu ya dondoo ya WHO inayohamasisha kutokomeza habari za uzushi za ugonjwa huo. 

Hadi sasa, kwa mujibu wa shirika hilo, ugonjwa huo umeshagharimu maisha ya watu zaidi ya milioni 1.2 ulimwenguni kote huku waliothirika wakifikia milioni 51.5.