November 24, 2024

Inawezekana kuongeza matumizi ya gesi kwa ajili ya kupikia

Ni kutengeneza mpango kabambe wa kuwawesha wananchi wa kipato cha chini kutumia gesi ya kupikia badala ya kuni na mkaa.

  • Ni kutengeneza mpango kabambe wa kuwawesha wananchi wa kipato cha chini kutumia gesi ya kupikia badala ya kuni na mkaa.
  • Kutoa ruzuku kwa ajili ya kupunguza gharama ya majiko ya gesi pamoja na mitungi ya gesi.
  • Kuondoa kodi katika majiko ya gesi, mitungi ya gesi na gesi yenyewe.

Hapa Tanzania, zaidi ya asilimia 85 ya Watanzania wote hutumia tungamotaka (biomass) kwa ajili ya kupikia ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya tani milioni mbili za mkaa hutumika hapa nchini kwa ajili ya kupikia kwa mwaka na karibu nusu ya matumizi hayo yapo katika Jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFSA), Tanzania ina eneo la misitu lipatalo hekari 48.1 milioni lakini hekari 370,000 za misitu zinaharibiwa au kukatwa kila mwaka kwa ajili ya matumizi ya nishati ikiwemo ya kuni na mkaa. 

Hii inamaanisha kuwa eneo lote la misitu linaweza kuwa limemalizwa baada ya miaka 100 ijayo ikiwa kasi hii ya uharibifu na ukataji miti kwa ajili ya nishati itaendelea.

Lakini bado tuna nafasi ya kuhifadhi misitu yetu isiharibiwe hasa kwa kugeukia matumizi ya gesi ya kupikia majumbani ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kuwa mbadala wa kuni na mkaa. 

Matumizi ya gesi (Liquified Petroleum Gas) yanaendelea kuongezeka hapa nchini. Inakadiriwa kuwa Tanzania iliingiza kiasi cha tani za ujazo (Metric Tonnes) 107,083 za gesi ya kupikia mwaka 2016/17 ukilinganisha na tani za ujazo 71,311 kwa mwaka 2015/16.

Ongezeko hilo ni sawa na asilimia 33.4 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ikidhihirisha kuwa ni mwanzo mzuri katika matumizi ya nishati mbadala. 

Hata hivyo, gharama kubwa ya mitungi ya gesi pamoja na gharama za kununua gesi yenyewe bado ni changamoto ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hasa wa kawaida kutumia gesi kwa ajili ya kupikia. 


Soma zaidi: Maoni: Tunaweza kuwapa fursa Watanzania wengi zaidi kwa nishati jadidifu


Matumizi ya gesi ya kupikia huonekana kama ni anasa na ni watu wenye kipato cha kati na juu wanaoweza kumudu gharama zake. Lakini bado tunaweza kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini nao wakatumia gesi ya kupikia.

Mei 2 hadi 3, 2019 nilihudhuria mkutano uliofanyika Jijini Cape Town, Afrika Kusini wa  “Energy Poverty” ulioandaliwa na Jukwaa la Kimataifa la Nishati (International Energy Forum) pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Nchi zinazozalisha mafuta duniani (OFID) uliokuwa ukizungumzia njia mbalimbali za kuondoa umasikini kwa kutumia nishati duniani.

Nishati ya kupikia ilichukuwa sehemu kubwa ya mijadala na tulijifunza jinsi serikali ya India ilivyowezesha wananchi wake hasa wa kipato cha chini kuanza kutumia gesi kwa ajili ya kupikia.

Hata hivyo, gharama kubwa ya mitungi ya gesi pamoja na gharama za kununua gesi yenyewe bado ni changamoto ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hasa wa kawaida kutumia gesi kwa ajili ya kupikia. Picha|Mtandao.

Kwa kushirikiana na waagizaji wa mafuta nchini India, Serikali nchini humo inatoa ruzuku kwa ajili ya kupunguza gharama ya majiko ya gesi pamoja na mitungi ya gesi. 

Umetengenezwa mpango kabambe wa uzambazaji gesi mpaka vijijini ambao unaenda sambamba na utoaji elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi na salama ya gesi. 

Watumiaji wote wa gesi waliofaidika na mpango huo wanaingizwa kwenye kanzidata (database) na wanafuatiliwa kuhakikisha hawarudi kwenye matumizi ya kuni.

Ni wakati sasa kwa Tanzania kufikiria namna ya kuwawezesha wananchi wake hasa wa kawaida kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na kuanza kutumia gesi. 

Tunaweza kuanza kwa kuondoa kodi katika majiko ya gesi, mitungi ya gesi na gesi yenyewe lakini pia tunaweza kwa kushirikiana na wadau wetu wa maendeleo kutengeneza mpango wa muda mrefu kwa kujifunza kutoka India. Inawezekana!

Prosper Magali ni Mtaalamu wa Nishati Jadidifu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 17, ni Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Nishati Jadidifu (Tanzania Renewable Energy Association) na mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa ya Alliance for Rural Electrification yenye Makao yake Makuu Brussels, Ubelgiji na pia Mkurugenzi wa Miradi na Ubunifu wa Kampuni ya Ensol Tanzania Ltd, waendelezaji miradi ya nishati jadidifu wa hapa Tanzania. Makala hii ni maoni yake binafsi.