November 24, 2024

Jack Ma akabidhi mikoba ya Alibaba kwa washirika wake

Mwanzilishi wa kampuni inayojihusisha na manunuzi ya mtandaoni ya Alibaba, Jack Ma ameachia ngazi rasmi kama Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo.

Anastaafu akiwa anatimiza miaka 55 huku akishikiria rekodi ya kuwa wa kwanza kwa utajiri nchini China kwa utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 38.4 (Sh88.3 trilioni) ikiwa ni kwa mujibu wa jarida la Forbes la Marekani. Picha| Mtandao.


  • Nafasi yake kama mwenyekiti wa kampuni ya Alibaba Group imechukuliwa na Daniel Zhang
  • Ataendelea kuwa mwanabodi wa kampuni hiyo hadi kikao cha 2020
  • Utumishi wake unabaki kwenye  ‘Alibaba Partnership’ kwa kipindi chote cha maisha yake.

Dar es Salaam. Mwanzilishi wa kampuni inayojihusisha na manunuzi ya mtandaoni ya Alibaba,  Jack Ma ameachia ngazi rasmi kama Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo.

Amemkabidhi mikoba yake rasmi, Daniel Zhang ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo inayokuwa kasi duniani. 

Ma aliachia ngazi kama Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo mwaka 2018 ambapo alimteua Zhang kukaimu nafasi hiyo na sasa Zhang ana kaimu nafasi ya uenyekiti wa kampuni hiyo.

Hata hivyo, Ma ataendelea kuwa mmoja wa wanabodi wa kampuni hiyo hadi mkutano wa wadau wa kampuni hiyo utakapokutana mwaka 2020.

Ma anabaki kuwa mdau wa “Alibaba Partnership” (kundi la viongozi wa ngazi ya juu wa Alibaba Group) kwa kipindi chote cha maisha yake akihusika katika kutoa mapendekezo yanayohusiana na kampuni hiyo. 

Ma anayeshika nafasi ya 21 katika orodha ya mabilionea duniani, mwaka 2018 wakati anajiaandaa kung’atuka alisema “hii ni ishara kuwa Alibaba inavuka kwenda hatua nyingine ya kiutawala kutoka ngazi ya kampuni inayotegemea mtu binafsi, kwenda juu ya mifumo ya ubora wa shirika na utamaduni wa maendeleo ya talanta.”


Zinazohusiana:


Ma aliachia ngazi kama Mkurugenzi Mtendaji wa Alibaba mwaka 2013 na kukabidhi majukumu hayo kwa Jonathan Lu ambaye pia mwaka 2015 aling’atuka na nafasi hiyo ikashikiliwa na Zhang ambaye alikua Mkuu wa Uendeshaji wa kampuni ya Alibaba Group.

Wakati akimwacha viatu vyake kwa Zhang huku watu mbalimbali wakijadili iwapo viatu hivyo vitamtosha endapo kasi ya soko la biashara ya mtandaoni nchini China itaendelea kusuasua.

Pamoja na majukumu aliyonayo Ma amezidi kuonesha shauku ya kujifunza mambo mbalimbali kwasababu ndicho kitu anachopenda kufanya zaidi katika maisha yake.

Kulingana na ripoti mbalimbali, Ma ni mwalimu mstaafu na mmoja ya waanzilishi wa Alibaba mwaka 1999. 

Anastaafu akiwa anatimiza miaka 55 huku akishikiria rekodi ya kuwa wa kwanza kwa utajiri nchini China kwa utajiri wa Dola za Marekani Bilioni 38.4 (Sh88.3 trilioni) ikiwa ni kwa mujibu wa jarida la Forbes la Marekani.