Jeshi la polisi lafafanua matumizi ya fataki mkesha wa mwaka mpya 2020
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amepiga marufuku wananchi kufyatua fataki bila kibali kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro hasa katika mkesha wa sherehe za mwaka mpya.
Wengine wamekuwa wakirusha fataki, baruti, kuimba au kupiga kelele na vyombo vya muziki kuonyesha furaha waliyonayo ya kuuona mwaka mpya. Picha|Mtandao.
- Lasema watakaofyatua fataki ni wale waliopata kibali cha polisi
- Lawataka kufanya ibada ya mkesha wa mwaka mpya kwa amani na kuepuka vurugu.
Dar es Salaam. Wakati zimebaki saa chache kumaliza mwaka 2019, kila mahali duniani, watu wanajiandaa kufanya matukio mbalimbali yatakayoashiria kuingia mwaka mpya wa 2020 ambao unasubiriwa kwa shauku.
Wengine wamekuwa wakirusha fataki, baruti, kuimba au kupiga kelele na vyombo vya muziki kuonyesha furaha waliyonayo ya kuuona mwaka mwingine. Lakini kama uko Tanzania na unataka kufyatua fataki jipange ili furaha yako itimilike.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amepiga marufuku wananchi kufyatua fataki bila kibali kutoka kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro hasa katika mkesha wa sherehe za mwaka mpya.
Mambosasa aliyekuwa akizungumza leo (Desemba 31, 2019) jijini Dar es Salaam, amesema jeshi hilo halitasita kumchukuliwa hatua za kinidhamu mwananchi yoyote atakayekiuka taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
“Wasiokuwa na kibali hawataruhusiwa kufyatua fataki na aliyepata kibali hicho ruksa kufyatua na tutamlinda lakini pia kuna mipaka yake, fataki ambazo zitakuwa na sauti kama mabomu ambayo yataleta taharuki hayataruhusiwa,” amesema Mombasasa.
Soma Zaidi:
- Jinsi ya kudhibiti matumizi mabaya ya pesa zako
- Namna ya kudhibiti matumizi mabaya ya pesa mwisho wa mwaka
Katika siku hii, watu hukusanyika katika maeneo ya wazi na nyumba za ibada ili kuukaribisha na kumshukuru Mungu kwa kuingia mwaka mpya.
Jeshi hilo limewataka wananchi kufanya ibada ya mkesha wa mwaka mpya leo Jumatano usiku kwa amani na kutahadharisha kuweka maeneo yao katika hali za usalama kabla hawajaenda kwenye ibada hiyo.
“Nawafahamisha kwamba jeshi la polisi tumeimarisha ulinzi maeneo yote ya ibada ambazo zinakuwa na mikesha kuelekea mwaka mpya ikiwamo uwanja wa Taifa na makanisa mbalimbali ambayo yametoa taarifa.
“Lengo ni kuhakikisha waumini wanafanya ibada hiyo wanakuwa salama. Lakini pia nitoe rai kwa wazazi, washerehekee sikukuu hii na familia zao, kuna baadhi ya wazazi wanaacha watoto wanazurura peke yao hii ni hatari,” amesema
Amesema jeshi hilo limejipanga kuimarisha ulinzi katika maeneo yote nchini Tanzania.