Jiandae kwa Nukta mpya mwaka 2020
Tutamwaga habari za data zilizochambuliwa kwa kina na kwa lugha rahisi kuwasaidia vijana kubaini fursa na kutatua changamoto zinazowakabili.
- Miongoni mwa mambo tutakayoboresha mwaka huu ni kujenga mifumo imara ya kiteknolojia ya kutoa habari itakayokuwa rafiki zaidi na simu janja.
- Tutamwaga habari za data zilizochambuliwa kwa kina na kwa lugha rahisi kuwasaidia vijana kubaini fursa na kutatua changamoto zinazowakabili.
Kwa miezi 24 sasa tumekuwa tukikuletea habari na makala mbalimbali kila siku kuhusu uchumi, teknolojia, takwimu, utalii, biashara na elimu kwa lugha yetu ya Taifa ya Kiswahili. Wakati wote huo tumejitahidi kuhakikisha tunakupatia uchambuzi unaoweza kukusaidia kufanya maamuzi katika biashara na maisha ya kawaida.
Kama chombo chochote cha habari kichanga tunapata faraja kuona kuna wasomaji wengi ambao haipiti siku moja bila kufungua tovuti yetu. Hii ni faraja kubwa kwetu. Tusipochapisha chochote hutupa mrejesho. Tukichapisha habari chini ya kiwango hawaachi kutueleza ukweli na hata tukifanya vyema hawasiti kutupongeza kuendeleza ubora huo.
Katika kipindi hicho cha miaka miwili jamii ya wasomaji wa Nukta imepaa mara dufu. Kukua kwa jamii hii inayotaka habari na makala makini zilizochambuliwa kwa kina ni ishara kuwa jumuiya ya watumiaji wa mtandao wanahitaji maudhui yenye manufaa kwao na Taifa.
Uwepo wa jamii ya aina hii inatupa wajibu wa kuendelea kufikiria kuzalisha na kuchapisha maudhui bora na ya kipekee ili kukidhi kiu ya wasomaji.
Mahitaji hayo na mirejesho kutoka kwa wasomaji yametufanya tuendelee kufanya ubunifu wa kimaudhui na kutafuta njia itakayofanya habari ziwafikie vijana kwa kasi zaidi na kupitia mifumo rafiki inayoendana na simu janja.
Soma zaidi:
- Jinsi ya kudhibiti matumizi makubwa ya pesa wakati wa mapumziko ya wikiendi
- Nukta Africa yateuliwa katika mpango wa Google
- Internews, Nukta Africa wafungua fursa ya mafunzo kwa wanahabari Tanzania
Ili kutimiza wajibu wetu wa kuzalisha maudhui yatakayosaidia vijana, kuanzia sasa tutaongeza zaidi maudhui kuhusu fursa za ajira, masomo, biashara, ubunifu mbalimbali na maarifa yatakayowasaidia kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuwakabili.
Tunaamini bila taarifa sahihi, mjadala na ushauri wenye weledi, inaweza ikatuchukua muda mrefu kufikia malengo ya kuwawezesha vijana kukua kiuchumi.
Kwa kuanza, mwaka 2020 tutaboresha tovuti zetu na akaunti zetu za mitandao ya kijamii ili kuhakikisha habari na makala zinawafikia wasomaji wetu katika mifumo yote ya maandishi, picha, video na infografia na kwa ubora wa hali ya juu.
Mbali na masuala ya teknolojia, safari hii tutajumuisha makala za uchambuzi na maoni kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo vijana na watu wengine wenye uzoefu wa kutosha kutatua changamoto za vijana hususan katika masuala tunayotilia mkazo ya kibiashara, takwimu, uchumi, teknolojia, elimu na utalii.
Si rahisi kueleza mambo yote tunayotarajia kuyafanya katika kuboresha uzalishaji na usambazaji wa habari zetu, lakini kwa kifupi tunakuomba ukae mkao wa kula. Nukta mpya inakuja.
Kheri ya mwaka mpya na endelea kusoma nukta.co.tz.
Picha ya mbele|Bram Naus/Unsplash.