Jinsi unavyoweza kutumia namba za utambulisho kuokoa simu iliyopotea
Husaidia katika kubaini simu iliyopotea na mahali ilipo ikiwa namba hizo zitatumika kikamilifu.
Umuhimu wa kufahamu tarakimu za IMEI ni mkubwa kwani unampa mhusika uwezo wa kutambua kifaa chake kwa njia ya kielektroniki. Picha | Mtandao.
- Zinatambulisha kifaa husika kwa mtumiaji pindi anapokuwa mbali na kifaa hicho.
- IMEI ni kiunganishi kati ya mitandao ya simu na mteja.
Dar es Salaam. Uwezo wa kutambua tarakimu za IMEI kwenye simu yako ni moja ya vitu muhimu kama mmiliki wa kifaa untakiwa kufahamu ili kukusaidia katika utambuzi pale anapotaka kujua kifaa hicho kilipo.
IMEI kwa kirefu chake ni “International Mobile Equipment Identity”. Ni namba ambazo zinakuwa kama utambulisho wa kifaa na katika simu, mara nyingi zinakuwa tarakimu15. Namba hizi huwa hazifanani na zinakuwa katika kifaa kimoja tu.
Umuhimu wa kufahamu tarakimu za IMEI ni mkubwa kwani unampa mhusika uwezo wa kutambua kifaa chake kwa njia ya kielektroniki hata asipokuwa na kifaa hicho kwa muda muafaka.
Ili mmiliki wa kifaa hicho aweze kupata tarakimu hizo kwenye simu; Anapaswa kwenda kwenye Mpangilio wa simu (Settings) kisha Kuhusu simu (About phone) ndipo ataona tarakimu za IMEI au kwa kupiga (*#06#) na kupata tarakimu anazoweza kunukuu na kutunza kwa manufaa yake ya baadae.
Tarakimu hizo pia husaidia kuzuia matukio ya wizi kwani kwa kutumia namba hizo, mara baada ya kuibiwa simu mhusika anaweza kuripoti polisi na kupata msaada wote wa namna ya kupata tarakimu hizo au kunasa mahali simu ilipo kwa wakati fulani.
Endapo itatokea simu imepotea na mhusika kukosa tarakimu hizo, hatua za awali ni kwenda kwenye kituo chochote cha polisi kwaajili ya kupata maombi yanayoenda kwenye kampuni husika kwaajili ya kupata namba hizo na kunasa mahala simu ilipo.
Mtaalamu wa masuala ya teknolojia kutoka mtandao wa simu wa Halotel, ameiambia www.nukta.co.tz kuwa kupata huduma ya kunasa simu pale itakapoibiwa ni haki ya kila mtanzania kinachohitajika ni kufuata taratibu zote za mchakato huo.
Amesisitiza kuwa umuhimu wa namba hizo ni mkubwa kwani ni kiunganishi kati ya mitandao ya simu na mteja.
“Moja ya jukumu ulilonalo kama mmiliki wa kifaa kama simu ni kujua IMEI namba. Zinasaidia sana hasa kwenye wizi. Tumeshasaidia wateja wengi kupitia namba hizo.” Amesema mtaalamu huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.