July 3, 2024

Jinsi ya kujikinga na Corona ukiwa saluni

Wamiliki wa saluni na Vinyozi wametakiwa kuwa na vifaa vya kunawia mikono na vitakasa mikono kwa wanaoingia na kutoka kuosha mikono yao.

  • Kuhakikisha unanawa mikono, kuvaa barakoa na kuepuka msongamano.
  • Kuwapima wateja wao joto la mwili kabla ya kuingia saluni kama inawezekana kufanya hivyo.
  • Kila mteja anatakiwa kutumia taulo lake lililo safi.

Dar es Salaam. Saluni ni sehemu muhimu ambayo watu husuka na kunyoa nywele ili kupata muonekano mzuri.

Hata hivyo, wataalam wa afya wanaeleza kuwa vinyozi na wasusi wanahitaji umakini mkubwa wakati wanatoa huduma ili kujikinga na kuwakinga wateja wao na Corona (Uviko-19).

Umakini huo unahitajika kwa sababu huduma hizo huambatana na kusogeleana na kugusana hasa kichwani, hivyo kuwa rahisi kusambaza maambukizi ya Uviko-19.

Kuhakikisha watumiaji wa saluni wanakua salama,  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa mwongozo unaoelekeza hatua za kufuata ili kujikinga na ugonjwa huo.

Mwongozo huo umetaja maeneo 12 ambayo yanatakiwa kuzingatiwa kwenye saluni na vinyozi huku mwongozo ukiagiza ukaguzi wa mara kwa mara wa maafisa wa afya wa halmashauri.

Wamiliki wa saluni na Vinyozi wametakiwa  kuwa na vifaa vya kunawia mikono na vitakasa mikono kwa wanaoingia na kutoka kuosha mikono yao.

Pia wanatakiwa kuwapima wateja wao joto la mwili kabla ya kuingia saluni kama inawezekana kufanya hivyo.

Kila kiti cha saluni kinatakiwa kiwe katika umbali wa mita moja na pale inaposhindikana wateja wasubiri nje ili kuepusha msongamano, inaeleza sehemu ya mwongozo huo ambao umesainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Abel Makubi Julai 25, 2021.

“Kuhakikisha uvaaji wa barakoa muda wote kwa watoa huduma na wateja. Barakoa hizi ziwe zinatumika mara moja kila baada ya masaa 4 na ivaliwe barabara kuhakikisha inafunika mdomo na pua,” unaeleza mwongozo huo.

Prof Makubi anasema katika mwongozo huo kuwa lazima kuwepo na taulo zilizofuliwa, kukauka na kupasiwa vya kutosha  kulingana na wingi wa wateja.

Sambamba na hilo kila mteja anatakiwa kutumia taulo lake lililo safi.

“Pale ambapo wateja watavishwa joho la kufunika mwili, mhudumu ahakikishe mteja amezungushiwa ‘tissue’ shingoni kabla ya kuvikwa joho hilo na tissue isitumike zaidi ya mara moja,” unaeleza mwongozo huo.

Sehemu ya nane ya mwongozo huo inaeleza kuwa wateja wenye joto kali la mwili, mafua na kikohozi wasiruhusiwe kuingia saluni huku wenyewe saluni wakitakiwa kuweka tangazo linalowataka walio na hali hiyo kwenda kupata matibabu kwenye vituo vya afya.


Watu wa ‘massage’ nao wapewa neno

Kwa upande wanaohudumia watoa huduma ya ‘massage’ au kuosha wametakiwa kuhakikisha wanavaa ‘gloves’ pamoja na barakoa muda wote wanapotoa huduma.

Pamoja na hilo pia wameelekezwa kuwepo na  chombo cha kuhifadhi taka na kuhakisha barakoa zote na ‘tissue’ zinachomwa.