October 7, 2024

Jinsi ya kujikinga na madhara ya ongezeko la joto Tanzania

Ni pamoja na kupunguza ulaji wa vyakula vilivyo na protini nyingi na kunywa maji kwa wingi

  • Ni kwa kunywa maji mengi na kuepuka matumizi ya baadhi ya vinywaji.
  • Punguza ulaji wa vyakula vyenye protini na kula zaidi matunda na mboga mboga. 

Dar es Salaam. “Usiku wa leo, sijalala kabisa, kila saa nashtuka na nikiamka nimeloa jasho. Hapa nina usingizi kama wote,” alisikika mwanamke mmoja akiongea na mwezake kwenye daladala leo Desemba 8, 2020 jijini Dar es Salaam.

“Hili joto siyo la kawaida, siyo asubuhi wala usiku,” anaendelea kusema mama huyo wa makamu katika daladala iliyokua ikitoka Kariakoo kuelekea Tegeta. 

“Hatuna jinsi ni majira yake haya, muhimu tuvae nguo nyepesi,” alijibu mwenzake ambaye alikua amekaa karibu na dirisha huku jua nalo likipenya kwenye gari na kuzidisha joto. 

Wanawake hao ni miongoni mwa watu wengi katika baadhi ya mikoa ya Tanzania ambao wanapata joto kali katika maeneo yao likiwemo jiji la Dar es Salaam.

Kwa nini joto linakua kali?

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine. 

“Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine,” imeeleza TMA katika taarifa yake iliyotolewa Desemba 8, 2020.

Nyakati za usiku, pia kunaonekana kuwa na hali ya joto kutokana na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani kinachofika asilimia 80 na zaidi kwa baadhi ya maeneo. 

“Unyevunyevu huo hutunza hali ya joto litokanalo na mionzi ya jua na hivyo kuleta hali ya fukuto,” imesema TMA. 

Unashauriwa kunywa maji mengi unapokuwa katika shughuli zako za kila siku ili kuhakikisha mwili unapata maji ya kutosha wakati wote. Picha| freepik.com.

Hata hivyo, hali ya joto inatarajiwa kupungua kidogo katika kipindi cha mwezi Januari, 2021 kutokana na mvua zinazotarajiwa katika baadhi ya maeneo. 

Aidha, vipindi hivi vya joto vinatarajiwa kuendelea kuongezeka katika mwezi Februari 2021 wakati jua litakapokuwa la utosi hapa nchini. Ili kukabiliana na ongezeko hilo la joto, fanya haya kujikinga na madhara zaidi:


Kunywa maji mengi

Katika kipindi cha joto, mwili hutoa jasho jingi na hivyo endapo mwili wako utaishiwa maji, huenda ukajikuta unadhoofu na kuwa na ngozi kavu.

Unashauriwa kunywa maji mengi unapokuwa katika shughuli zako za kila siku ili kuhakikisha mwili unapata maji ya kutosha wakati wote.

Kama hauwezi kukumbuka kunywa maji, nunua chupa maalumu kwa ajili ya kubebea maji ili ikukumbushe kunywa maji pale unapoiona. Zipo programu za mtandaoni (Apps) ambazo unaweza kuzitumia kukukumbusha kunywa maji  kufikia lengo utakalolihitaji.


Soma zaidi:


Punguza ulaji wa vyakula vilivyo na kiwango kikubwa cha protini

Vyakula kama nyama nyekundu ikiwemo ya mbuzi na ng’ombe vinasababisha mwili kutoa joto jingi wakati wa umeng’enyaji hivyo ulaji wake huenda ukakuongezea sintofahamu juu ya joto lililopo.

Badala yake pendelea kutumia matunda na mboga mboga. Kwa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka, matunda yapo mengi na yanapatikana kwa bei rahisi sokoni.


Punguza matumizi ya vinywaji vyenye kafeini 

Vinyaji vilivyo na kafeini kama chai na kahawa unatakiwa kuviepuka katika msimu huu wa joto kwani vinachochea mwili kupoteza maji. Kwa vinywaji, unashauriwa kutumia vinywaji vilivyo na vitamini C ili kuiboresha kinga yako ya mwili dhidi ya magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa ya joto. 

Pia punguza matumizi ya vinywaji vikali kama pombe.